KENYA inaingia katika kipindi nyeti cha kiuchumi huku ikikaribia Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, wakati changamoto kadhaa za uchumi zikiendelea kuathiri maisha ya wananchi na utulivu wa nchi. Licha ya kuwepo kwa dalili za ustahimilivu katika baadhi ya viashiria vya uchumi, wananchi wengi bado wanakabiliwa na ukuaji hafifu, mzigo wa madeni, ukosefu wa ajira na kupungua kwa mikopo kwa sekta binafsi.
Kwa mujibu wa makadirio yaliyotolewa katika Kongamano la Mtazamo wa Uchumi wa 2026 lililoandaliwa na Kenya Private Sector Alliance (KEPSA), uchumi wa Kenya unatarajiwa kukua kati ya asilimia 4.9 hadi 5.2 mwaka 2026.Hata hivyo, kiwango hicho bado kiko chini ya wastani wa kihistoria wa takribani asilimia 6. Pamoja na takwimu hizo kuonesha matumaini ya kuimarika kwa uchumi, wananchi wengi bado hawajafaidika ipasavyo. Sekta ya kilimo, inayowaajiri wananchi wengi hasa vijijini, imekua kwa asilimia 3.2 tu, hali inayoendelea kubana kipato cha wakazi wa maeneo hayo. SOMA: Deni la Taifa Kenya laongezeka
Kadiri uchaguzi wa 2027 unavyokaribia, tafiti zinaonesha wananchi wengi wana wasiwasi kuhusu hali ya maisha na mustakabali wa uchumi. Utafiti wa TIFA Research unaonesha asilimia 67 ya familia zinaamini hali yao ya kifedha imekuwa mbaya zaidi tangu uchaguzi wa 2022, huku asilimia 49 wakiamini uchumi utaendelea kudorora mwaka 2026.

Changamoto nyingine kubwa ni deni la taifa na gharama zake za kulihudumia. Taasisi za kimataifa zimeonya kuwa Kenya iko katika hatari kubwa ya kushindwa kumudu madeni, huku sehemu kubwa ya mapato ya serikali ikitumika kulipa riba badala ya kugharamia huduma muhimu kama miundombinu, elimu na afya.
Wakati huo huo, ukosefu wa ajira, hasa kwa vijana, pamoja na kupanda kwa gharama za maisha vinaendelea kuwabana wananchi wengi licha ya kupungua kwa mfumuko wa bei kwa ujumla. Aidha, maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 yanakabiliwa na changamoto za kifedha baada ya Tume ya Uchaguzi nchini humo kueleza kuwepo kwa upungufu wa bajeti wa takribani shilingi bilioni 22.9, jambo linaloweza kuathiri baadhi ya shughuli za maandalizi ya uchaguzi.
Kwa sasa Kenya inaingia katika kipindi muhimu ambapo uchumi na siasa vinaingiliana kwa karibu. Wataalamu wanaeleza kuwa bila maboresho ya haraka katika maisha ya wananchi, changamoto za kiuchumi zinaweza kuongeza presha za kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027.