
Katika ziara ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba inayoendelea mikoa mbalimbali, tunashuhudia akitatua na kuzipatia ufumbuzi papo kwa hapo, kero zinazowakabili watanzania lakini hili linathibitisha ombwe la taasisi imara.
Ninasema hivyo kwa sababu kuna kero au changamoto zingine zingeweza kutatuliwa na wateule wengine wa Rais kama wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa Halmashauri, maofisa ardhi au hata watendaji wa kata.
Lakini kama kero na matatizo ya watanzania yale ambayo sio ya kisera, yanasubiri hadi Rais au waziri mkuu afanye ziara ndio yapate ufumbuzi basi hapo kuna tatizo na tena tatizo lenyewe ni kukosekana kwa taasisi imara kuanzia ngazi za chini.
Yaani mpaka kero hiyo afikishiwe Rais au Waziri mkuu katika mkutano wa hadhara kunaonyesha kuwa mtumishi wa umma ambaye hatimizi majukumu yake na madhara yake ni kwamba lawama zitaenda kwa Rais na chama tawala.
Tunapozungumzia taasisi imara sio ofisi kama zile za wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya au wakurugenzi wa Halmashauri pekee, la hasha, bali ni pamoja na Bunge, Mahakama na vyombo kama Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya aina hiyo.
Ukisoma Ibara ile ya 35(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inasema Shughuli zote za utendaji za Serikali ya Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na watumishi wa Serikali kwa niaba ya Rais.
Kwa hiyo kuna kero ambazo zinapelekwa kwa waziri mkuu katika ziara zake ambazo zingeweza kuwa zimetatuliwa na watumishi wa umma walioko kwenye ofisi za umma na wanaolipwa mishahara kwa kodi za watanzania masikini.
Ndio maana nimetangulia kusema ziara ya Dk Mwigulu na kero au changamoto anazopelekewa kuzitatua na zingine ndogo tu ambazo zingeweza kutatuliwa na maofisa ardhi, kunadhihirisha uwepo wa ombwe la taasisi imara.
Ukisoma Ibara ya 52 ya Katiba ya Tanzania inasema Waziri Mkuu atakuwa na madaraka juu ya udhibiti, usimamiaji, utekelezaji wa siku hata siku wa kazi na shughuli za Serikali na ndiye atakuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni.
Katika utekelezaji wa madaraka yake, Waziri Mkuu atatekeleza au kusababisha utekelezaji wa jambo lolote au mambo yoyote ambayo Rais ataagiza kwamba yatekelezwe na atawajibika kwa Rais kuhusu utekelezaji wa madaraka yake.
Serikali chini ya mamlaka ya Rais, ndiyo itakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi juu ya sera ya Serikali na Mawaziri, chini ya uongozi wa Waziri Mkuu,watawajibika kwa pamoja Bungeni kuhusu utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Ndio maana watanzania walio wengi wanaililia Katiba mpya sio kuitumia kama silaha kuing’oa Serikali ya CCM madarakani, la hasha, ni ili itengeneze taasisi imara na huru na mifumo ya uendeshaji wa nchi, ambayo kila mmoja atawajibika.
Lengo la 16 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya Umoja wa Mataifa (UN) ni kukuza jamii zenye amani na jumuishi, kuhakikisha upatikanaji wa haki kwa wote, na kujenga taasisi imara zenye uwajibikaji na ufanisi katika ngazi zote.
Kwa hiyo lengo hili ambalo linatakiwa limetimizwa ifikapo mwaka 2030, linalenga kupunguza vurugu, kupambana na rushwa, na kuimarisha mifumo ya sheria, hasa kwa nchi zinazokabiliwa na misukosuko ya kisiasa na utawala mbovu.
Huu sio mwelekeo mzuri, tunahitaji kuwa na taasisi imara (strong institutions), zenye watendaji na watumishi wa umma wenye weledi na ujuzi na wanaotekeleza wajibu wao kwa kumsaidia Rais kama ibara ile ya 35 ya Katiba inavyosema.
Kwa hiyo utatuzi ule wa kero na changamoto unaofanywa na Dk Mwigulu katika mikutano yake si jambo la kufurahia, bali lituamshe (wakeup call) kutoka usingizini kwamba tunahitaji taasisi imara na huru ambazo zitamsaidia Rais kuoingoza nchi.
Mathalan, migogoro ya ardhi au haki mirathi ambayo imekuwa changamoto kubwa nchini zingeweza kupatiwa ufumbuzi na wakurugenzi wa Halmashauri, Maofisa Ardhi, wakuu wa mikoa na wilaya bila kusubiri ujio wa waziri mkuu.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali imepanga kutumia Sh10.2 trilioni kulipa mishahara ya watumishi wa umma, ikiwa ni sawa na wastani wa Sh 856 bilioni kwa mwezi. Hizi ni fedha nyingi sana na tunapaswa kuziona katika utendaji wao.
Ndio maana nasema tunahitaji Taasisi imara kumpunguzia Rais au waziri mkuu mzigo wa kutatua kero ndogondogo kwani changamoto nyingi anazokutana nazo Dk Mwigulu zingetatuliwa kupitia mifumo thabiti ya utendaji wa taasisi imara.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. Anapatikana kwenye namba 065660090