Madrid, Hispania. Hofu imetanda ndani ya kikosi cha Real Madrid baada ya nyota wao, Kylian Mbappé, kuripotiwa kuwa katika hatari ya kuukosa mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica.
Mbappe, ambaye ndiye kinara wa mabao wa Madrid msimu huu akiwa na mabao 38 katika michuano yote, inadaiwa amekuwa akicheza kwa maumivu makali ya goti la kushoto kwa takribani wiki sita sasa.
Ripoti kutoka vyombo vya habari vya Ulaya zinaeleza kuwa mshambuliaji huyo amekuwa akicheza kwa mguu mmoja, akipata shida hasa anapohitaji kuongeza kasi au kubadili mwelekeo.
Mshambuliaji wa Real Madrid, Kylian Mbappé ambaye anaripotiwa kuwa na maumivu ya goti la kushoto. Picha na Mtandao
Nyota huyo wa zamani wa Paris Saint-Germain (PSG) tayari amefunga mabao 13 katika Ligi ya Mabingwa msimu huu.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa madaktari wa klabu pamoja na mchezaji mwenyewe wana wasiwasi juu ya utayari wake kwa mechi ya marudiano itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Taarifa zinaonya kuwa kama ataendelea kulazimisha kucheza, huenda akahitaji mapumziko ya siku 10, jambo litakalomfanya akose michezo muhimu ya La Liga dhidi ya Getafe na Celta Vigo wakati Madrid wakiwania ubingwa dhidi ya Barcelona.
Nyota wa Real Madrid, Kylian Mbappé, wakati akionekana kuzidiwa na maumivu ya goti la kushoto alipokuwa kwenye uwanja wa mazoezi. Picha na Mtandao
Katika mazoezi ya wazi Jumanne, Mbappe alionekana kushiriki lakini alishindwa kumaliza kipindi chote kutokana na maumivu ya goti.
Licha ya hali hiyo, kocha wa Madrid, Álvaro Arbeloa, ameonyesha matumaini makubwa kuwa mshambuliaji huyo atakuwa tayari kucheza.
“Kylian yuko tayari kwa mechi ya leo, hilo ndilo muhimu zaidi kwa sasa. Ameonyesha kujitoa kwa timu na anaweza kuamua mchezo wakati wowote,” amesema Arbeloa.
Kocha wa Real Madrid, Álvaro Arbeloa, akizungumzia hali ya mshambuliaji wake, Kylian Mbappé. Picha na Mtandao
Sakata la ubaguzi latia doa mechi
Mchezo huo unakuja pia ukiwa bado umefunikwa na sakata la tuhuma za ubaguzi dhidi ya mshambuliaji wa Madrid, Vinícius Júnior.
Katika mchezo wa kwanza, kiungo wa Benfica, Gianluca Prestianni, alidaiwa kutumia neno la kibaguzi “mono” (tumbili) baada ya Vinicius kufunga na kusherehekea bao. Prestianni amekanusha madai hayo, lakini tayari amepewa adhabu ya muda ya mechi moja na Shirikisho la Soka barani Ulaya (UEFA) wakati uchunguzi ukiendelea.
Winga wa Real Madrid, Vinicius Jr (akiwa kushoto) katika mgogoro na nyota wa Benfica, Gianluca Prestianni wakati akidai kutolewa maneno ya kibaguzi katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao
Mbappe alikuwa mmoja wa waliomsimamia hadharani Vinicius baada ya mechi hiyo, akisisitiza kuwa hakuna binadamu anayestahili kufanyiwa vitendo vya kibaguzi.
“Sijawahi kuamini kuwa kuna mtu anayestahili kufanyiwa mambo kama haya,” alisema Mbappe.
Sasa macho yote yanaelekezwa Santiago Bernabeu, ambapo Madrid wanahitaji kulinda ushindi wao wa bao 1-0, huku afya ya Mbappe ikiwa kitendawili kikubwa kabla ya dakika 90 za maamuzi.