Dar es Salaam. “Asante, rubani wetu! Asante, mwanamke wa shoka, kwa kutufikisha salama salmini! Mungu akubariki sana!”

Haya ni baadhi ya maneno yanayosikika kutoka kwa abiria wakimpongeza Joyce Foya kila anapowafikisha salama mwisho wa safari zao.

Kauli hizo si za kawaida katika usafiri wa daladala, jijini Dar es Salaam, bali ni ishara ya heshima na kuthamini juhudi za mwanamke aliyethubutu kuingia katika taaluma inayoonekana kutawaliwa zaidi na wanaume.

Joyce (33), ni dereva wa daladala inayofanya safari kati ya Soko la Kigogo, lililopo Pugu, Wilaya ya Ilala, na Tandika, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.

Katika mahojiano ya takribani saa tatu na mwandishi wa makala hii, anasimulia kwa kina safari yake ya maisha hadi kufikia hapo alipo, changamoto anazokutana nazo barabarani pamoja na mafanikio aliyoyapata kupitia kazi hiyo.

Anasema tangu akiwa mdogo alikuwa na ndoto ya kuwa dereva, lakini changamoto za maisha zilimlazimu kupita njia ndefu kabla ya kufikia ndoto hiyo.

Dereva wa daladala, Joyce Foya akiendesha daladala jijini Dar es Salaam.

Kwa mara ya kwanza alifika jijini Dar es Salaam mwaka 2010, akitokea mkoani Kilimanjaro, kwa lengo la kumsaidia dada yake katika duka la biashara. Alihudumu kwa mwaka mmoja kabla ya kuamua kuacha kazi hiyo baada ya kutofautiana na dada yake katika masuala kadhaa, na kurejea Kilimanjaro.

Mwaka 2012, alirejea Dar es Salaam. Safari hii aliishi kwa rafiki yake na kuanza kutafuta kazi. Alipata kazi kwa mama lishe maarufu mama ntilie katika eneo la Mwembe Yanga, Wilaya ya Temeke, ambapo alikuwa akipika na kuuza chakula.

“Nilipokuwa nafanya kazi hiyo, baadhi ya madereva na makondakta waliokuwa wakija kula niliwaeleza nia yangu ya kuwa dereva. Wengine waliniambia si rahisi, na kwamba nianzie kwanza kazi ya ukondakta,” anasema Joyce.

Mwaka 2016 kuelekea 2017, ndipo alipoanza kazi ya ukondakta. Anasema alipata nafasi hiyo kwa bahati, baada ya dereva mmoja kumchukua kwa dharura siku ambayo aliyekuwa akimshika alikuwa na tatizo.

“Haikuwa rahisi kuingia kwenye kazi hii. Nilijiapiza kwamba nikishapata nafasi sitafanya makosa. Nakumbuka mara ya kwanza nilianza kwenye gari la Kariakoo–Temeke, kwa sababu wakati huo ruti ya Buza–Kigogo zilikuwa hazijaanza,” anasema.

Anakiri kuwa hakukuwa na jambo lililomuumiza kama kuona baadhi ya makondakta wa kiume wakiingia kazini kwa muda mfupi, kisha kufundishwa udereva hadi kuwa madereva kamili, wakati yeye hakuaminika kuwa anaweza.

“Nilizoea kazi taratibu hadi nilipopata dereva wa gari la Kigogo–Tandika. Huyu ndiye aliyenifundisha kuendesha gari,” anasema.

Anaeleza kuwa mafunzo hayakuwa mepesi. Wakati mwingine dereva huyo alikuwa akimkosoa kwa ukali, hata kumpiga makofi alipofanya makosa barabarani.

Hata hivyo, Joyce anasema hakukata tamaa kwa sababu alijua anachokitafuta. Alitaka kuvunja dhana iliyokuwepo kwamba wanawake hawawezi kuendesha daladala.

Baada ya kujifunza kwa vitendo, alikwenda darasani kusoma na kupata cheti pamoja na leseni ya udereva. Kwa sasa ana leseni inayomruhusu kuendesha hata mabasi makubwa.

Anasema amefikisha miaka mitatu tangu aanze rasmi kazi ya udereva, na uzoefu alioupata alipokuwa kondakta umemsaidia kuifahamu barabara na mbinu za kazi.

Changamoto barabarani

Joyce anasema, pamoja na mafanikio, anakumbana na changamoto kutoka kwa madereva wenzake, abiria, na hata wananchi wa kawaida.

Kwa upande wa madereva wenzake, anasema wakati mwingine wanapomwona amepakia abiria wengi na kuwazidi, baadhi yao hutoa maneno ya dharau.

“Wapo wanaosema, ‘Hizi sasa dharau, demu anajazaje kunishinda?’ Pia wapo ambao nikiwapita barabarani wanakasirika na kuamua kutosimama kuchukua abiria, hata kama wapo kituoni, ilimradi tu nisiwapite,” anasema.

Kwa upande wa abiria, anasema, mbali na wale wanaompongeza, wapo wanaotoa kauli za kejeli.

“Wengine husema, ‘kazi za kupika mmemwachia nani hadi mje kuendesha magari?’ Lakini maneno hayo huwa nayapuuza. Nilishayazoea tangu nikiwa kondakta. Nimejifunza kutokujali nani atasema nini. Kikubwa ni kwamba naipenda kazi yangu na nimeipambania,” anasisitiza.

Anakumbuka pia kuwa mwanzoni baadhi ya abiria walipogundua dereva ni mwanamke walishuka wakidai hawawezi kuendeshwa na mwanamke. Hata hivyo, kadiri muda ulivyopita na watu kuona uwezo wake, hali hiyo imepungua kwa kiasi kikubwa.

Mtazamo wa familia

Anasema kwa upande wa familia, mwanzo haikuwa rahisi, kwani wazazi na ndugu zake hawakukubaliana naye kufanya kazi ya ukondakta, wakihofia ataingia katika mazingira yasiyofaa.

Dereva wa daladala, Joyce Foya, akizungumza na mwandishi wa habari wa gazeti la  Mwanachi, Nasra Abdalla katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam.

Hali hiyo iliendelea hata alipoanza udereva. Anasema aliwahi kutuma video kwenye kundi la familia la Whatsaop akionesha akiwa kazini, lakini mmoja wa kaka zake alimwonya, akidhani anachezea magari ya watu.

“Hata nilipomwambia nimekuwa dereva rasmi, hakuniamini. Alienda hadi kumuuliza mwanangu anajua mama yake anafanya kazi gani. Mtoto alipomwambia ni dereva, alimhoji iwapo nimetuma adanganye,’” anasema kwa tabasamu.

Baadaye, familia ilimtuma dada yake kusafiri kutoka Kilimanjaro hadi Dar es Salaam ili kujionea. Baada ya kuthibitisha, ndipo walipoanza kumuunga mkono na kutambua kuwa ni kazi halali kama zilivyo nyingine.

Majukumu ya mama na kazi

Joyce ni mama wa mtoto wa kiume anayesoma darasa la saba. Awali aliishi naye Dar es Salaam, lakini alipofika darasa la nne alimpeleka kuishi kwa mama yake mkubwa Moshi, ili apate mazingira tulivu ya masomo. Kwa sasa, mtoto huja kwake wakati wa likizo.

Anasema amejiwekea ratiba madhubuti ya kazi; huanza saa 11:00 alfajiri na kurejea nyumbani saa 11:00 jioni. Jumamosi na Jumapili ni siku zake za mapumziko.

Ratiba hiyo humwezesha kupata muda wa kukaa na mtoto wake anapokuwa likizo, pamoja na kushiriki shughuli za kijamii.

Mafanikio na matarajio

Kupitia kazi yake, Joyce anasema amejenga nyumba eneo la Chanika kwamba anajivunia mafanikio hayo kwa kuwa yametokana na jasho lake mwenyewe.

Katika matarajio yake, anatamani kumiliki gari lake binafsi la abiria, sasa ameanza kuweka akiba ili kufanikisha ndoto hiyo.

Anasema, kama angepata fursa ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, moja ya maombi yake yangekuwa kupata msaada wa kufanikisha azma ya kumiliki chombo chake cha usafiri.

Wanasemaje wenzake?

Baadhi ya madereva wanaofanya kazi naye katika ruti hiyo wanasema Joyce ni mfano wa kuigwa.

Juma Pazzy, anasema mbali na kuwa dereva mwenzao, kwao ni kama kiongozi, kwani mmiliki wa gari amemuamini kiasi cha kumkabidhi mapato ya kila siku.

“Hii inaonesha kwamba mwanamke akiaminika, anaaminika kweli. Wanawake wengine wenye ndoto kama zake wasione aibu kuingia katika fani hii. Kila jambo linawezekana kwa juhudi,” anasema.

Hussein Mkelemi, naye anasema wanamuona Joyce kama mwanamke aliyethubutu kufanya jambo tofauti.

Anasema wanashirikiana naye vizuri si tu katika kazi ya udereva, bali pia katika masuala ya kijamii.

Kwa upande wake, kondakta anayefanya kazi na Joyce, aliyejitambulisha kwa jina la Farida Iddi, anasema anajisikia fahari kufanya kazi na dereva mwanamke. Anasema Joyce amempa hamasa ya kutamani siku moja awe dereva pia.

Hadithi ya Joyce oya ni ushuhuda kwamba ndoto hazina jinsia. Ni simulizi ya uthubutu, uvumilivu na kujiamini katika mazingira yanayoweza kukatisha tamaa.

Kupitia juhudi zake, amevunja vikwazo vya kijamii na kuwa mfano hai wa mwanamke anayeweza kusimama imara katika taaluma yoyote, mradi awe na dhamira na bidii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *