Juzi, Fyatu mmoja aliyefyatuka bila aibu wala woga akanifyatua na kuzusha kuwa nina uroho wa madaraka kana kwamba yeye hanao! Nani asiyependa madaraka? Kwanza, sikuamini ningehusishwa na dhambi hii ambayo chanzo chake ni shetani kutaka kumfyatua Sir God aliyemfinyanga asijue.

Huwa nashangaa. Kwanini Sir God ‘mjua yote’ hakujua kuwa sheitwan angejaribu kumfyatua? Siishii hapo. Kifyatufyatu, hujiuliza. Kama kweli sheitwan ‘alipanga’ kumfyatua Sir God, ilikuwaje tukatupiwa sisi na si aliyemfyatua?

Tuache ngano za imani kama zile za imani ya amani. Yawezekana sheitwan ni Gen Ziro kama siyo zero brain. Sheitwan ashindwe na kulegea au atokomezwe akatokomee mbali watoi wapone. Ashindwe sawa na wale wanaoteka, kupoteza, na kuua ili wote wenye ufyatu tupone.

Ashindwe pamoja na watesi wetu wanaojifanya kuwa wapenzi wetu. Nilijishangaa na kuwashangaa mafyatu fyatuliwa na fyatuzi waliofyatuliwa na wale wasioamini wasingeweza kufyatuka tukafyatuana.

Si ni pale ‘mamluki’ wachochezi waliohongwa na mabeberu na mafahari walipofyatuka wakafyatua na ‘kuwachochea Gen Ziro wetu na kukikunisha hadi wote kunuka tusijue tulikuwa tunawapinga na kuwasweka ndani waliotabiri kuwa kingenuka kikanuka!

Je, nani astahiki kushikwa na kuswekwa lupango kati ya waliosema kingenuka na waliokinukisha? Anayebisha, kupata jibu sahihi na ukweli, akamuulize Toto Tunda Lishe na wale waliomfyatua kwa kuzuia asiwafyatue wakaishia kufyatuliwa na kuaibika wasijue namna ya kujisafisha.

Hapa, mwenye makosa ni waliofyatuka wakafyatua au wale walio fyatuka wakawafyatua waliokataa kufyatuliwa wakitaka kuzuia wasifyatuliwe? Lazima tufyatuke na kutaka kujua mwenye makosa ili tumfyatue kutoa somo kwa yeyote atakayepanga au kudhamiria kutufyatua siku zijazo.  Kweli mambo yamebadilika!  Hakuna ufyatu ulionitisha na kunichukiza kama kusikia mafyatu tena wanene wakifyatuka bila aibu kuwa hakuna waliouawa wakati ushahidi unafyatua vinginevyo? Je, hapa nani anamfyatua nani ili iweje kama siyo kujifyatua ufahamu na kuongeza mafuta motoni? Unajifunza nini hapa?

Hakuna kitu kilinifyatua nikafyatuka na kutamani kufyatua kama kusikia eti waliofyatuka wakakinukisha walikuwa mamluki! Hivi, kweli waliofyatuka hadi damu zikajaa kila mahali kayani kweli walikuwa mamluki? Kama ni kweli, waliowaua walikuwa nani?

Fyatu ningependa kujua hao ‘mamluki’ wazandiki waliingiaje kayani bila vyombo vya uhasama, sorry, usalama kujua hadi wasiwafyatue kabla ya kuingia na kutufyatua kama ‘walivyotufyatua?’Hayo tuyaache. Mgoshi Machungi umeipata au unjifanya chura usisikie japo wasikia?

Hakika, nilisikia watuhumiwa wa unyotoaji roho na ukatilii wakitoa ‘nsamaha’! Eti wanataka marudiano sijui maridhishano! Kilichotoka hakiwezi kurudi. Hamkani si shwari tena. Maji yeshamwaika. Hii ni kweli, inawezekana, au ni gea?

Je, tunaanzaje ‘kusameheana’ hata kusemezana mbali na kuridhiana na kuridhishana bila kujua nani alifanya nini na kwanini na iwe nini? Nani mwenye mamlaka au kawapa mamlaka au ni kujipa mamlaka bila kuweka wazi nani anamsamehe nani na kwa mamlaka na uhalali vipi?

Ukisia uchokozi wa kiwango cha SGR, ndo huu. Hivi, huwa unajisikiaje pale aliyekukosea na kukufyatua anapojifyatua ufahamu na kukataa au kushindwa kukuomba msamaha huku akijibaraguza kwa kukubagaza kuwa ‘anakusamehe’ kana kwamba hakukukosea? Nani wa kusamehe na kusamehewa hapa? Unasamehewa kwa makosa gani wakati mkosewa ni wewe? Je, nani apaswa kumhukumu, kumsamehe, hata kumuadhibu nani? Hebu tufyatuke kiakili na kuuliza. Je, ni nini chanzo cha haya manukishano? Kwani, hatujui chanzo na sababu au tunajifyatua ufahamu tukidhani na wahanga nao watatufuata wajifyatue badala ya kutufyatua kwa kuwafyatua?

‘Wasio’ waroho wa madaraka wanatuhimiza tuchukie wanaowapinga kwa sababu wana uroho wa madaraka! Ni uroho upi wa madaraka kati ya walioyapata kwa mlango wa nyuma na wanaoyatafuta kwa kufuata haki zao kikatiba? Nini uroho na usio uroho?

Nani asiyependa madaraka huyu tumuone atufunze jambo au mawili tuache uroho wa madaraka? Je, kupenda au kutafuta madaraka ni uroho wa madaraka au ndiyo maana na roho ya madaraka? Nani asiye mroho wa madaraka aliye tayari kuyaachia bila kuyang’ang’ania ukiachia mbali kuyapoka hata kwa kuua wenzake?

Hakuna kilichonishangaza kama kusikia walioamuru mauaji ya halaiki ya mamluki ‘wakihuzunika’ midomoni wakati rohoni wanafurahi! Ajabu ya maajabu ni pale mtuhumiwa anaposamehe na kuunda (timu siyo tume) eti kujichunguza kama njia ya kuwafyatua mafyatu!

Je, mafyatu wataigia mkenge wafyatuliwe kirahisi hivi? Nani apaswa kuunda timu au hata tume kati ya aliyenyotoa roho na aliyenyotolewa roho? Hivi, yupo awezaye kuridhiana na marehemu?

Ukifanya hivyo na ndugu zake, ujue wao siyo yeye wala hawajui angefanya au kusema nini kuhusiana na kunyotolewa roho bila hatia zaidi ya wahuni na waroho fulani kutaka au kung’ang’ania madaraka kinyume cha sharia, kikatili, na kizwazwa? Nimewasamehe ‘mamluki wote’ walionifyatua. Hivi, niko wapi, nafanya nini, na nimesema nini?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *