MOROGORO :Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa uwekezaji wa zaidi ya Sh bilioni 700 uliofanywa na Kilombero Sugar Company Limited una mchango mkubwa katika kupunguza changamoto ya ajira nchini, hususan katika sekta nyeti za uhandisi na taaluma nyingine za kiufundi.
Prof. Mkumbo ametoa kauli hiyo jana alipofanya ziara katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, na kutembelea kiwanda hicho cha sukari.

Akiwa katika ziara hiyo ya kikazi, ameeleza kuwa uwekezaji huo umefungua ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, amesema kuwa sekta ya viwanda ina nafasi muhimu katika kukuza uchumi wa Taifa na kuimarisha ajira kwa vijana, hasa wale wenye ujuzi wa kitaaluma na kiufundi.
Amebainisha kuwa uwekezaji mkubwa kama huo si tu unaongeza uzalishaji wa bidhaa muhimu kama sukari, bali pia unachochea maendeleo ya sekta nyingine zinazohusiana nazo, ikiwemo kilimo cha miwa, usafirishaji na huduma za usambazaji.
Aidha, Prof. Mkumbo amewataka wawekezaji wengine nchini kuiga mfano wa Kiwanda cha Sukari Kilombero kwa kutoa kipaumbele kwa wazawa katika ajira, akisisitiza kuwa rasilimali watu wa ndani wanapaswa kunufaika moja kwa moja na miradi ya uwekezaji inayofanyika nchini.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza ukosefu wa ajira, kuongeza kipato kwa wananchi na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.
Katika hatua nyingine, waziri huyo ameongeza kuwa Tanzania kwa sasa imepiga hatua kubwa katika kujitosheleza kwa uzalishaji wa sukari, kwa kuwa awali kiwanda hicho kilikuwa kinazalisha kati ya tani 130 hadi 260, lakini kutokana na maboresho ya miundombinu, teknolojia na upanuzi wa uzalishaji, kiwango hicho kimeongezeka kwa kiasi kikubwa na kusaidia kukidhi mahitaji ya soko la ndani.
Amesisitiza kuwa kuongezeka kwa uzalishaji wa ndani kunapunguza utegemezi wa uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi, kuimarisha usalama wa chakula na malighafi za viwandani, pamoja na kuchangia ukuaji wa pato la taifa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kufuatilia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, kuhakikisha uwekezaji una tija kwa taifa, na kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayovutia wawekezaji zaidi katika sekta za uzalishaji na viwanda.