
Dar es Salaam. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) umeivunja Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) Tanzania, kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa mali za kanisa na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Februari 25, 2026 jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Rita, Frank Kanyusi, amesema uamuzi huo umetokana na matokeo ya ripoti maalumu ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyowasilishwa kwa wakala huo.
Amesema ukaguzi huo maalumu ulifanyika baada ya wanachama wa kanisa hilo kuwasilisha malalamiko wakidai kuwepo kwa vitendo vya ukiukwaji wa pamoja vya wajumbe wa bodi, ikiwemo ubadhirifu wa mali za kanisa.
“Ripoti imebaini mapungufu makubwa katika utekelezaji wa majukumu kwa mujibu wa sheria, ikiwemo usimamizi mbovu wa mali za kanisa,” amesema Kanyusi.
Amefafanua kuwa uamuzi wa kuivunja bodi umezingatia matakwa ya sheria, huku akiongeza kuwa ripoti ya CAG itawasilishwa kwa vyombo vingine vya dola kwa hatua zaidi za kisheria.
Kanyusi amesema pia kanisa limepewa siku saba kuwasilisha Rita majina ya wajumbe 10 watakaounda kamati ya muda itakayoratibu shughuli za zake hadi uteuzi wa bodi mpya ya wadhamini utakapofanyika.
Msajili wa Jumuiya katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Emmanuel Kihampa, amesema ofisi yake imepokea malalamiko kadhaa kutoka kwa waumini wa kanisa hilo, yakiwemo madai ya ubadhirifu wa mali na kutowasilishwa kwa taarifa za mwaka kama inavyotakiwa na sheria.
Amesema migogoro ndani ya taasisi za kidini mara nyingi huanza kama malalamiko ya kawaida, lakini yasipotatuliwa mapema hugeuka migogoro mikubwa yenye athari kwa taasisi na jamii.
“Yasipotatuliwa mapema hugeuka migogoro rasmi, na yakichelewa kushughulikiwa husababisha mgawanyiko na kuvuruga amani,” amesema Kihamba.
Ameonya kuwa migogoro isiyopatiwa ufumbuzi ndani ya taasisi za kidini inaweza kusababisha mpasuko wa ndani, migawanyiko na hatimaye kuvunjika kwa amani.