
BAADA ya Tanzania Prisons kufikia makubaliano ya pande mbili kuachana na Kocha Zedeckia Evans Otieno, inaelezwa iko katika hatua nzuri ya mikoba yake kumkabidhi Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’ kutoka kwa maafande wa Transit Camp.
Taarifa ya Tanzania Prisons kuachana na Otieno iliyotolewa leo Februari 25, 2026 na Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Godfrey Madegwa, imesema:
“Uongozi wa timu ya Tanzania Prisons Football Club unapenda kuutaarifu umma kuwa, kwa makubaliano ya pande zote mbili, umefikia makubaliano ya kuachana na aliyekuwa Kocha Mkuu, Zedeckia Evans Otieno.”
“Aidha, Uongozi wa Tanzania Prisons Football Club unamshukuru Kocha Otieno kwa mchango na huduma yake kwa kipindi chote alichoitumikia timu na unamtakia kila la heri katika majukumu yake.”
Kuhusu Nsajigwa, kiongozi mmoja wa Transit Camp aliyeomba kuhifadhiwa jina lake, alisema ni kweli, kocha huyo yupo hatua za mwisho za kujiunga na Prisons, kwa sababu ya ushirikiano wa taasisi hizo mbili nchini.
“Timu zetu zote zinaendeshwa kwa misingi ya kijeshi, ambapo baada ya viongozi wenzetu kuonyesha uhitaji huo kwa ajili ya kuinusuru timu tulimruhusu, leo ilikuwa ni siku nzuri pia ya kuwaaga wachezaji kikosini,” kilisema chanzo hicho.
Kiongozi huyo alisema tangu Nsajigwa alipojiunga na kikosi hicho mwanzoni mwa msimu huu wa 2025-2026, akitokea Namungo alipokuwa msaidizi wa Kocha, Juma Mgunda, kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchezaji ambayo yameibadilisha timu hiyo.
Katika miaka ya mwanzoni ya taaluma yake, Nsajigwa aliwahi kuichezea Tanzania Prisons ya Mbeya, kisha kujiunga na Yanga aliyoitumikia kuanzia mwaka 2006 hadi mwaka 2012, huku pia akiwa ni nahodha wa kikosi cha timu ya taifa ya Taifa Stars.
Kwa msimu huu wa 2025-2026, Nsajigwa, ameiacha Transit Camp inayoshiriki Ligi ya Championship ikishika nafasi ya nne na pointi 37, baada ya kucheza mechi 19, ikishinda 11, sare minne na kupoteza pia minne, ikifunga mabao 26 na kuruhusu 17.
Kwa upande wa Zedekiah aliyejiunga na Prisons Julai 24, 2025, kwa msimu wa 2025-2026, ameiongoza timu hiyo katika mechi 14, za Ligi Kuu, ambapo kati ya hizo ameshinda tatu, sare tatu na kupoteza nane, ikifunga mabao manane na kuruhusu 16.
Katika mechi hizo 14, Otieno ameiacha Prisons ikiwa nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara na pointi zake 12, huku Mkenya huyo akizifundisha pia Gor Mahia FC, Sony Sugar, Posta Rangers na KCB FC zote za kwao Kenya na timu ya taifa ya Kenya maarufu ‘Harambee Stars’.