Dar es Salaam. Makada wa Chama cha Wananchi (CUF) wamesema uamuzi wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa wa kubatilisha uchaguzi wa ndani ya chama hicho, uliofanyika Desemba 18, 2024, umetenda haki kwa wanachama na wote waliogombea.
Uchaguzi huo uliomweka madarakani Profesa Lipumba na wenzake watano, ulikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa makada wengine waliowania nafasi hiyo, wakidai kwamba haukuwa huru na wa haki.
Msajili aliamua kutowatambua viongozi waliochaguliwa kwenye uchaguzi huo kwa sababu hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa, hivyo akabatilisha uchaguzi huo na kuagiza kwamba urudiwe.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama Cha Wananchi (CUF), wakati wa uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho uliofanyika Februari 21, 2026 baada ya uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kutengua uchaguzi uliofanyika mwaka 2024 na kumrejesha madarakani Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti, pamoja na wenzake watano. Picha na Maktaba
Uchaguzi wa marudio ulifanyika Februari 22, 2026 ambapo Mirambo Yusuf alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho, baada ya kupata kura 257 kati ya 448 zilizopigwa na wajumbe wa Baraza Kuu la CUF.
Akizungumza na Mwananchi leo Februari 25, 2026 kuhusu uamuzi wa Msajili kutaka uchaguzi huo kurudiwa kada wa CUF, Wilfred Lwakatare amesema sababu zilizotolewa na Ofisi ya Msajili, ndizo ambazo walizilalamikia awali lakini zikapuuzwa na kamati ya uchaguzi ya CUF, iliyosema hakukuwa na dosari katika mchakato huo.
Lwakatare aliyekuwa mmoja wagombea uenyekiti katika uchaguzi wa Desemba 18,2024 amesema alikuwa ni miongoni mwa walioandika barua ya malalamiko kuhusu mchakato huo, akidai kutoridhishwa ulivyoendeshwa.
“Niliwaambia haya mambo yamekosewa hapa, wakaniambia hakuna kasoro wala nini basi nikakaa kimya…Sasa nikapata taarifa kuna wagombea wengine waliandika barua kwenda ofisi ya Msajili.”
Wajumbe wa kikao cha Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF) wakiwa katika kikao hicho kinachoendelea makao makuu ya Chama hicho Buguruni, Dar es Salaam.
“Kasoro za uchaguzi ule zilitokea na kuonekana mapema, lakini fukia fukia zilizozoeleka zikachukua mkondo wake.Mambo yalitakiwa yamalizike mapema kutokana na kasoro tulizozibainisha, lakini zikapuuzwa jambo ambalo ni tabia mbaya,” ameeleza Lwakatare.
Katika uchaguzi huo wa Desemba 18, 2024 Lwakatare alipata kura 78 kati ya kura halali zilizopigwa huku Profesa Lipumba akiibuka kidedea kwa kupata kura 216.
Hata hivyo, katika mchakato huo Lwakatare alitangaza mara mbili kutogombea endapo jina la Lipumba litakuwepo, lakini ghafla alibadili gia angani na kuwania nafasi hiyo, akidai kuwashawishiwa na wajumbe waliokuwa wakimuunga mkono.
Katika hatua nyingine, Lwakatare amesema anawaombea Mungu viongozi wa sasa wa CUF wakae vizuri kwa maelewano ili chama hicho kisonge mbele, huku akimuomba Lipumba kuonyesha ustaarabu na usomi wake wa kukisaidia chama.
“Awape mawazo yake ya kukisaidia na kuboresha chama na awape maoni yatakayowasaidia viongozi wapya. Asitupe jongoo na mti wake, anapaswa kukisaidia chama na viongozi wapya,” amesisitiza Lwakatare.
Lwakatare aliyewahi kuwa mbunge wa Bukoba Mjini (Kagera) kwa nyakati tofauti amesema matatizo yanayoisumbua CUF yanajulikana, hivyo kwa siku chache alizomsikiliza Mirambo ameona kuna mwanga mbeleni.
Mwingine atia neno
Aliyekuwa mtiania wa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi wa Desemba 18, Jafar Mneke amesema mchakato huo uligubikwa na dosari kadhaa ndio maana alitangaza kujitoa mapema baada ya kuzibaini.
“Kweli kabisa kuna mambo hayakuwa sawa katika ule uchaguzi (Desemba 18) kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya ndani ya chama. Tulipofika katika uchaguzi mkuu nilipoona miongozo na kanuni imekiukwa na mwelekeo si mzuri nikajitoa.”
“Walioendelea na uchaguzi, baada ya mchakato kukamilika walikuja kuniambia kwamba nilichokisema kilikuwa sahihi kuhusu mambo kukiukwa. Waliniomba tuungane pamoja kupinga nikawakatalia kwa sababu awali walishindwa kunielewa,” amesema Mneke.
Kwa mujibu wa Mneke, moja ya mambo waliolalamikia wagombea hao ni hatua kitendo cha Profesa Lipumba kutangazwa mshindi pasipo kufikisha asilimia 51 kama kanuni za chama hicho zilivyoelekeza.
Ameongeza kuwa kanuni za chama hicho zinaelekeza uchaguzi urudiwe kwa kushindanisha aliyeshika nafasi ya kwanza na pili, endapo yatatokea mazingira ya mshindi kutofikisha asilimia 51, jambo ambalo halikufanyika.
Hivyo, walisimamia hoja hiyo na ile ya Lipumba kutofuata utaratibu wakati wa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ambapo walizifikisha kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
“Nashangaa kwa nini uamuzi huu umechelewa au umechukua muda mrefu kwa sababu mambo yalikuwa wazi. Hata hivyo, mwisho wa siku ofisi ya msajili imeona malalamiko yalikuwa halali na haki imetendeka,” ameeleza.
“Msajili yupo sahihi nilitarajia majibu haya yangekuja mapema, sijui kwa nini amechelewa kuyatoa maana kila kitu kilikuwa wazi kabisa. Hatuwezi kuikosoa CCM (Chama cha Mapinduzi) kwamba inakiuka taratibu wakati sisi wenyewe ndani ya chama hatufuati demokrasia wala haki hatutendi,” amesema.