
Mwanza. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) imekubali ombi la washtakiwa katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Salaaman Health Services Ltd, Abdi Warsame, na Ofisa Rasilimali Watu, Elia Makongwa, kufanya majadiliano na makubaliano ya kumaliza kesi (plea bargaining).
Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, Erick Maley, mahakama imepanga kukutana na pande zote mbili kwa ajili ya majadiliano yatakayofanyika Machi 4, 2026.
Washtakiwa hao wanaokabiliwa na mashtaka 841, wako mahabusu, walifikishwa mahakamani hapo jana, Jumanne, Februari 24, 2026, wakikabiliwa na mashtaka yanayojumuisha kuusababishia Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni kati ya mwaka 2021 na 2023, kupitia genge la uhalifu lililodaiwa kufanya kazi mkoani Mwanza na Dar es Salaam, pamoja na kutumia nyaraka za uongo.
Kesi hiyo, namba 2330 ya mwaka 2026, ilitajwa kwa mara ya kwanza Februari 4, 2026, na baadaye Februari 10, mbele ya Hakimu Maley.
Awali, akizungumza mahakamani hapo, Wakili wa Serikali, Fadhili Mwandoloma, amesema wamepokea maelekezo kupitia ofisi ya DPP kuendelea na mazungumzo kama upande wa utetezi ulivyoomba.
Hakimu Maley amesema mahakama imepanga kukutana na pande zote mbili Machi 4, mwaka huu, siku ambayo kesi hiyo itatajwa kwa ajili ya kupokea taarifa ya majadiliano.
Akizungumza baada ya shauri kuahirishwa, wakili wa utetezi, Allan Robi, amesema wamefurahishwa na uamuzi huo kwa kuwa una manufaa kwa pande zote mbili na utaokoa muda wa mahakama na gharama kwa Serikali.
Shauri la msingi
Katika kesi namba 2330 ya mwaka 2026, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka yanayojumuisha kuongoza genge la uhalifu, kughushi na kutumia nyaraka za uongo, wakidaiwa kupokea Sh1.011 bilioni, huku wakijua kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.
Wanadaiwa kughushi nyaraka za wagonjwa na kuzitumia kujipatia fedha isivyo halali kutoka ofisi za NSSF, jijini Dar es Salaam kwa madai ya kutoa huduma za matibabu katika Kituo cha afya Salaaman kilichopo mkoani Mwanza.
Kesi ilipotajwa Februari 10, Hakimu Maley aliiahirisha hadi Februari 24, 2026 baada ya kutoa uamuzi mdogo kuhusu ombi la matibabu kwa mshtakiwa wa kwanza, Dk Warsame.
Alielekeza mamlaka za magereza kuhakikisha mshtakiwa huyo anapatiwa huduma ya afya kwa mujibu wa taratibu.