Unguja. Serikali imesema inatambua umuhimu wa ukuaji wa biashara mtandaoni kama chachu ya maendeleo ya uchumi, upanuzi wa masoko na uongezaji wa ajira.
Imesema kwa ufahamu huo, ndiyo sababu imechukua hatua za kimkakati kuhakikisha biashara hizo zinatambulika rasmi na kupewa mazingira bora ya kustawi.
Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni kutungwa kwa Sera ya Biashara ya Zanzibar ya mwaka 2024, ambayo imeainisha biashara mtandaoni kuwa eneo la kipaumbele katika mikakati ya maendeleo ya sekta ya biashara visiwani humo.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Februari 25, 2026 na Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Mohammed Sijamini Mohamed, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Chake Chake, Abdulwahab Said Abuubakar (CCM).
Swali hilo lilitaka kufahamu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kutambua rasmi biashara za mtandaoni pamoja na mipango ya kuhakikisha wafanyabiashara hao wanalipa kodi na tozo stahiki.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Mohamed amesema wizara imetunga Sera ya Kidijitali ya Zanzibar ya mwaka 2026, ambayo imeweka mikakati ya kuendeleza biashara mtandaoni katika sekta zote za kipaumbele, ili kuongeza ufanisi, kupanua masoko na kuwezesha ukuaji wa biashara ndogondogo za kielektroniki.
Amesema pia Serikali imeandaa Mwongozo wa Uchumi wa Kidijitali Zanzibar wa mwaka 2023/2027, ambapo biashara mtandaoni imejumuishwa kama mojawapo ya vyanzo vya kuongeza mapato ya Serikali.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, sera hizo zimezingatia umuhimu wa kuunga mkono maendeleo ya biashara mtandaoni kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.
Aidha, Mohamed amesema teknolojia na ubunifu vimetambuliwa kuwa nyenzo muhimu za kuongeza thamani ya bidhaa, kuboresha ufungaji na kukuza biashara kwa njia ya mtandao.
Amesema pamoja na fursa zinazotokana na ukuaji wa biashara mtandaoni na matumizi ya majukwaa ya kidijitali pamoja na mitandao ya kijamii, bado kunahitajika mfumo thabiti wa ukusanyaji wa kodi na tozo stahiki ili kuimarisha mapato ya umma.
Katika kuimarisha usimamizi wa kodi, Mohamed amesema mwaka 2024 Serikali ilifanya marekebisho ya Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 1998, ili kuendana na mahitaji ya sasa ya ukusanyaji mapato katika sekta ya kidijitali.
Amesema Sheria ya Fedha (Usimamizi wa Mapato ya Umma) ya mwaka 2024, kwenye kifungu cha 4(A) na 4(B), yamewekwa masharti yanayohusu usajili na ulipaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa wafanyabiashara wasio na makazi au ofisi ya kudumu Zanzibar, wanaotoa huduma za kielektroniki.
Amesema sheria hiyo inawataka watoa huduma za kielektroniki wasio na makazi au ofisi ya kudumu Zanzibar, kujisajili katika Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) na kulipa VAT kwa mapato wanayopata kutokana na shughuli za kiuchumi, kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na hatua hizo za kisheria, Serikali inaendesha kampeni za uhamasishaji na utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara wanaotumia majukwaa ya kidijitali na mitandao ya kijamii, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wao wa kulipa kodi na kutumia mifumo ya malipo ya kidijitali.
Amesema lengo ni kuhakikisha wafanyabiashara wanafahamu majukumu yao ya kodi, manufaa ya kulipa kwa wakati, na namna mifumo ya kidijitali inavyoweza kuongeza usalama na urahisi katika malipo.
Kwa ujumla, Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha biashara za mtandaoni zinatambuliwa rasmi kupitia sera, mikakati na mifumo madhubuti ya kidijitali, sambamba na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya umma kwa maendeleo ya Zanzibar.