Barcelona, Hispania. Kiongozi wa bodi ya Barcelona, Joan Soler, amesema kuwa klabu hiyo inaweza kumsajili nyota wa Manchester City, Erling Haaland, licha ya changamoto za kifedha zinazoikabili klabu hiyo.
Barcelona imekuwa ikihusishwa na matatizo ya kifedha kwa miaka ya hivi karibuni, lakini Soler ambaye ni mjumbe wa bodi chini ya rais Joan Laporta, amesisitiza kuwa klabu iko tayari kufanya uwekezaji mkubwa dirisha lijalo la usajili.
Mshambuliaji wa Man City, Erling Haaland, (kushoto) mwingine ni mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez ambao wanawindwa na Barcelona katika dirisha lijalo la kiangazi. Picha na Mtandao
Akizungumza na chombo cha habari cha Cadena Ser, Soler amesema:
“Ndiyo, tunaweza kusajili wachezaji kama Julián Álvarez au Erling Haaland. Usajili huo utajilipa ndani ya miaka mitano, na hali ya kifedha ya Barcelona iko tayari kwa hilo.”
Hata hivyo, ameongeza kuwa klabu lazima iwe makini na mfumo wa mishahara:
“Tumejiwekea ukomo wa mishahara na hatutauvuka. Lazima tusajili kwa bei ya soko huku tukidhibiti matumizi.”
Mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez ambaye anawindwa na Barcelona katika dirisha lijalo la kiangazi. Picha na Mtandao
Safu ya ushambuliaji ni kipaumbele
Kocha Hansi Flick anatajwa kutaka kuimarisha safu ya ushambuliaji, wakati Robert Lewandowski, akiwa katika miezi ya mwisho ya mkataba wake.
Ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa Alvarez ndiye chaguo namba moja kwa Barca, lakini bei ya pauni 130.8 milioni inayotajwa na Atlético Madrid ni kikwazo kikubwa.
Kutokana na hilo, Barcelona inaangalia mbadala nafuu zaidi kwa mshambuliaji wa Man City, Omar Marmoush. Inadaiwa kuwa Barcelona walikuwa wanamtaka Marmoush alipokuwa Eintracht Frankfurt kabla kutua City kwa pauni 67 milioni Januari mwaka jana.
Mshambuliaji wa Man City, Omar Marmoush, anayeripotiwa kuwa chaguo lingine la Barcelona katika dirisha la usajili la kiangazi. Picha na Mtandao
Ingawa Marmoush hajapata nafasi kubwa chini ya Pep Guardiola msimu huu akiwa amecheza dakika 895 pekee katika mechi 24 (wastani wa dakika 37 kwa mechi) na kufunga mabao mawili lakini Flick anaamini ana sifa za mshambuliaji wa kisasa: mwenye kasi, anayeweza kucheza popote mbele na mwenye uwezo wa kufunga.
Barcelona wana matumaini kuwa wanaweza kumpata kwa bei ya chini kuliko ile City waliomnunua.