
Dar es Salaam. Kesi ya mfanyakazi wa ndani wa Uganda, Vicky Ajok, aliyohukumiwa kifo nchini Syria alikokuwa akifanyia kazi hiyo, imeibua mjadala wa maisha ya wafanyakazi wa ndani wakiwemo wanaosafiri kwenda mataifa ya nje.
Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari kutoka nchini humo na BBC, jijini Damascus, Vicky alipatikana na hatia ya kumuua mwajiri wake mwenye umri wa miaka 87, Huda Shaarawi, ambaye taarifa ni msanii maarufu nchini humo anayefahamika kupitia tamthilia ya Bab Al Hara.
Katika maelezo yaliyosambazwa kupitia vyombo vya habari vya ndani, Vicky anadaiwa kutenda kosa hilo baada ya mabishano makali kati yake na mwajiri wake, yaliyopeleka Vicky kumpiga kwa kitu kizito na kusababisha majeraha yaliyopelekea kifo, kisha kutoroka kabla ya kukamatwa na vyombo vya usalama ambapo alidai kuwa alikuwa akinyanyaswa kwa muda mrefu ikiwemo kutolipwa mshahara kwa muda mrefu.
Aidha, kupitilia video iliyosambaa ikimuonyesha Vicky akiwa chini ya ulinzi, akieleza tukio na kuomba msamaha huku akilia, imezua mjadala kuhusu mazingira ya kukiri kwake kosa na kama alipata uwakilishi wa kisheria wa kutosha. Hukumu hiyo imepangwa kufanyika Februari 28, 2026, huku wito wa kusitishwa kwa adhabu hiyo ukiendelea.
Nchini Tanzania, maelfu ya wanawake wa Kitanzania huenda Mashariki ya Kati kila mwaka kufanya kazi za ndani, wengi wao kupitia mikataba ya mawakala binafsi bila uelewa mpana wa haki zao au mazingira halisi ya kazi wanazokwenda kukutana nazo.
Katika baadhi ya nchi, mfanyakazi wa ndani huwa chini ya udhamini wa mwajiri, hali inayoweza kujumuisha kushikiliwa kwa hati za kusafiria au kuzuiwa kuondoka bila idhini, hivyo madai ya Vicky kutolipwa mshahara na kunyanyaswa yanaonesha uwepo wa ukatili na mazingira magumu kwa watu hawa huko nje.
Katika mitandao ya kijamii, wadau wameibua mawazo mseto wakirejea kisa cha Vicky kama tukio linalopaswa kutazamwa kwa umakini mkubwa kuhusu namna ya uratibu wa kazi hizi, wakiwemo Watanzania wanaofanya kazi kama hizi nje ya nchi.
Kwa upande wao, wadau na mawakala wa haki za wafanyakazi wa ndani nchini wamekuwa na maoni mseto wakitaja vyanzo vikuu vya migogoro ya wafanyakazi wa ndani na waajiri wao, tahadhari na namna ya kushughulikia matatizo haya kwa ndani na wanaokwenda nje ya nchi.
Tatizo huanzia hapa
Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wadada Consultant Center, Amani Ramadhani anasema kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo ya ukatili hutokana na namna waajiri wanavyoishi na wafanyakazi wao.
Anasema baadhi wanawachukulia wasichana wa kazi kama watu duni na kuwatendea kama siyo sehemu ya familia.
“Inategemea sana unavyoishi na mfanyakazi wako. Ukimchukulia kama sehemu ya familia na si mtu wa kazi tu, hata akiwa na changamoto itakuwa rahisi kukuambia kuliko kuchukua maamuzi ya hasira,” anasema.
Anabainisha kuwa baadhi ya waajiri hawatengi muda wa kumsikiliza mfanyakazi wao kujua hali yake, changamoto anazopitia au hata hisia zake. Anataja pia visa vya unyanyasaji wa kingono vinavyowakumba baadhi ya wasaidizi wa nyumbani, hasa kutoka kwa waajiri wa kiume.
Katika mazingira ambayo mfanyakazi hajajengewa ukaribu wa kuzungumza na mwajiri wa kike au hana pa kuripoti, hujikuta akibeba maumivu peke yake jambo linaloweza kuzaa hasira na maamuzi mabaya.
Mbali na hilo, ucheleweshwaji wa mishahara bila sababu za msingi, vipigo, matusi au fedheha mbele ya watoto na majirani, amevitaja kuwa miongoni mwa sababu zinazochochea migogoro.
“Unapomcheleweshea mshahara miezi miwili au mitatu bila maelezo, au kumjibu kwa ukali kila anapouliza haki yake, unajenga chuki. Wengine hufikia hatua ya kuona bora liwalo na liwe,” anasema.
Suluhu ni kuwathamini, kulinda haki zao
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Majumbani, Zanini Athumani amesema ili kuondokana na matukio hayo mfanyakazi mwenyewe anatakiwa kujitambua kuwa yeye ni nani, haki zake pamoja na majukumu yake.
Pia, amesisitiza ni muhimu kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, huku waajiri wakiwapa thamani na kutimiza stahiki zao kwani wanayo nafasi ya kipekee ndani ya nyumba kwa kuwa wao ndio husimama kama wasimamizi wa familia pindi mama anapokuwa katika majukumu ya kikazi.
“Kuna baadhi ya waajiri huwachukulia wasichana kama watu maskini waliotoka familia duni hivyo wanaweza kuwafanya chochote watakacho, mtazamo huo si mzuri na wanatakiwa kuachana nao mara moja,” amesema.
Amesema ni muhimu kwa waajiri kuishi na wasichana hao wa kazi kwa upendo na kuwapa faraja kwani baadhi yao wametoka katika mazingira waliokuwa wakifanyiwa ukatili.
Pia, amesisitiza wasaidizi wa nyumbani kuwa na hofu ya Mungu hata inapotokea kutoelewana na waajiri wao wasichukue hatua ya kulipa visasi kwa wasio na hatia, bali wahakikishe wanafuata taratibu zilizowekwa kisheria.
Wanaosafirishwa nje
Wazna Seif Suleiman, Mkurugenzi Mkuu wa Al bashir Recruitment and Travel Agency Limited, inayoratibu wafanyakazi wa ndani kwenda nchi za Mashariki ya Kati, amesema wanaowasafirisha wasaidizi hao wa nyumbani wana wajibu wa kusimamia ustawi wa wafanyakazi hao ikiwa ni pamoja na kuhakiki mikataba yao, kufuatilia haki zao, stahiki zao na kujenga ukaribu na balozi na taasisi za Serikali.
Anasema kwa kufanya hivyo, huweza kujua kile kinachoendelea kwa wafanyakazi hao na kusaidia kutatua changamoto zinazojitokeza kabla hazijaleta madhara.
“Hawa wanaokwenda nje huwa chini ya uangalizi wa taasisi husika inayowasafirisha. Sisi tunawasimamia kuanzia mikataba yao na wanapokuwa na shida ndio huwa wa kwanza kuwasaidia kwa kuwa tunawajibika na kila kitakachowapata.
“Pia, huwa tunawafundisha kuwa wawazi kwetu wanapohisi kuna jambo huko haliko sawa na tunawaunganisha na ofisi za mabalozi na Wizara ya Kazi. Kwa kufanya hivyo hatujawahi kusikia wala kupata tatizo kwa watu wetu huko nje,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mgono Housemaid, Christopher Mgono amesema baadhi ya migogoro hiyo huanzia kwa mwajiri kushindwa kuweka mazingira rafiki na ya haki kwa mfanyakazi wa ndani, akiwataka waajiri kubadili mtazamo na kuishi na wafanyakazi wao kama sehemu ya familia ili kuepuka chuki, visasi na madhara yanayoweza kuzuilika.
Amesema zama zimebadilika na wasaidizi wa nyumbani wa sasa wanafahamu haki zao zaidi kutokana na maendeleo ya teknolojia na mitandao ya kijamii, hivyo waajiri wanapaswa kuwa waangalifu na kuzingatia utu.
“Zamani wasaidizi wengi walikuwa na hofu na hawakuwa wakitambua haki zao, lakini sasa dunia imebadilika. Ni muhimu mwajiri kumchukulia dada wa kazi kama mwanafamilia, si kama mtumwa,”
Nyongeza na Mariam Mbwana