Manchester, England. Nahodha wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, ameitaka klabu hiyo kuanza haraka mchakato wa kumtafuta kocha mwingine wa kudumu badala ya kumpa nafasi hiyo Michael Carrick, licha ya mwanzo wake mzuri tangu achukue mikoba ya Ruben Amorim.

Carrick aliteuliwa kuwa kocha wa muda Januari baada ya kuondolewa Amorim, kwa mkataba unaoisha mwishoni mwa msimu. Tangu arejee Old Trafford, United wameshinda mechi tano kati ya sita za Ligi Kuu England na kutoka sare moja, na kupanda hadi nafasi ya nne wakibaki pointi tatu tu nyuma ya Aston Villa katika nafasi ya tatu.

Miongoni mwa ushindi wao ni dhidi ya Manchester City na Arsenal, jambo lililowafanya mashabiki wengi kutaka Carrick apewe kibarua cha kudumu.

Nahodha wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, amesema United wanapaswa kumchagua kocha mwenye wasifu bora zaidi. Picha na Mtandao

Hata hivyo, akizungumza katika kipindi cha Sky Sports, Neville amesema United wanapaswa kumchagua kocha mwenye wasifu bora zaidi ili kupunguza hatari.

“Si kwamba nipo dhidi yake. Nampenda sana Michael na amefanya kazi kubwa hadi sasa. Lakini Manchester United wanapaswa kwenda kwa kocha wa kiwango cha juu zaidi anayepatikana,” amesema Neville.

Ameongeza kuwa klabu hiyo tayari imejaribu makocha vijana au wasio na uzoefu mkubwa katika chaguzi zao mbili zilizopita bila mafanikio ya kudumu, akitoa mfano wa kurejea kwa Ole Gunnar Solskjær, ambaye alianza vizuri lakini hakumaliza vyema.

Neville pia ameonya kuwa chaguo kadhaa zinaweza kupungua, akitaja uamuzi wa Thomas Tuchel kusaini upya mkataba wake na timu ya taifa ya England kuwa unapunguza wigo wa United.

Kocha wa muda wa Man United, Michael Carrick, ambaye ameonyesha mwendelezo mzuri wa matokeo ndani ya Klabu hiyo ya Old Trafford. Picha na Mtandao

United kufuzu Ligi ya Mabingwa

Pamoja na msimamo wake huo, Neville anaamini Carrick ana uwezo wa kuipeleka United kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao.

Amesema timu nyingi zinazowania nafasi nne za juu zina majukumu ya michuano ya hiyo, hali ambayo inaweza kuwachosha na kupoteza pointi, wakati United hawana usumbufu huo.

“Naamini wanaweza kumaliza wa tatu au wa nne. Ni msimu wa ajabu, timu zinapoteza pointi bila kutarajiwa. United sasa wako katika nafasi nzuri,” amesema.

Amekiri kuwa miezi michache iliyopita hakuamini kama United wanaweza kuwania nafasi za Ligi ya Mabingwa, lakini mabadiliko ya matokeo yamewapa matumaini makubwa.

Kwa sasa, United wanaonekana kushika usukani katika mbio za nne bora, lakini mjadala kuhusu nani atakayekuwa kocha wa kudumu unaendelea kupamba moto ndani na nje ya Old Trafford.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *