Licha ya kuwepo kwa mafanikio katika umiliki na usimamizi wa ardhi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, ni asilimia 35 tu ya ardhi ya dunia ndiyo ina nyaraka rasmi za umiliki, hali inayosababisha watu kuwa na hofu ya kupoteza maeneo yao.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya hali ya umiliki na usimamizi wa ardhi iliyotolewa leo  mjini Rome, Italia na Cartagena de Indias, nchini Colombia, ikibainisha kuwa kasi ya kurasimisha ardhi imekuwa ndogo mno ikilinganishwa na mahitaji.

Ripoti hiyo iliyoandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), inasema kuwa ukosefu wa nyaraka unadhoofisha uwekezaji wa muda mrefu na uhakika wa chakula.

Wanawake kumiliki ardhi bado ni changamoto

Hali ni mbaya zaidi kwa wananchi wa kawaida ambapo takriban watu bilioni 1.1, sawa na mtu mmoja kati ya kila watu wazima 4  duniani, wanaishi kwa hofu ya kupoteza ardhi zao ndani ya miaka mitano ijayo.

Ripoti imefichua kuwa wanaume wana uwezekano mkubwa zaidi wa kumiliki au kuwa na haki salama za ardhi kuliko wanawake katika nchi karibu zote zilizofanyiwa utafiti. Hali ya kusikitisha ni kwamba, pengo la kijinsia katika umiliki wa ardhi linazidi asilimia 20 katika karibu nusu ya nchi zote zenye takwimu, jambo linalowaacha wanawake wakiwa hatarini zaidi kiuchumi.

Haki za wanawake katika umiliki wa ardhi nchini Kenya.

Haki za wanawake katika umiliki wa ardhi nchini Kenya.

Kusini mwa jangwa la Sahara umiliki wa ardhi wazingatia mila

Katika nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, asilimia 73 ya ardhi inamilikiwa kwa kufuata mifumo ya kimila, ni asilimia 1 pekee ndiyo inayotambuliwa rasmi kisheria. Hali hii inawaacha mamilioni ya watu katika hatari ya kupoteza maeneo yao kutokana na upanuzi wa miji na miradi mikubwa ya uwekezaji.

Marcy Vigoda, Mkurugenzi wa Muungano wa Kimataifa wa Ardhi (ILC), amesisitiza, “watu wengi sana bado wanaishi na hofu ya kupoteza ardhi na nyumba zao, huku wanawake na vijana wakibaki miongoni mwa waliotengwa zaidi, uhalisia unaodhoofisha uhakika wa chakula na hatua za mabadiliko ya tabianchi.”

Matajiri wanamiliki eneo kubwa la ardhi

Ripoti hiyo pia imefichua ukosefu wa usawa katika ugawaji wa ardhi ya kilimo ambapo asilimia 10 ya wamiliki wakubwa wa ardhi wanamiliki asilimia 89 ya ardhi yote ya kilimo duniani. Wakati huo huo, asilimia 85 ya wakulima wadogo duniani wanamili chini ya hekta mbili kila mmoja, sawa na asilimia 9 pekee ya ardhi ya kilimo duniani kote.

Mchumi Mkuu wa FAO, Maximo Torero Cullen, amesema, “Ukosefu wa uhakika wa ardhi ni aina hatari sana ya ukosefu wa usawa, matokeo yake ni uzalishaji mdogo wa mazaounao, kukosa ustahimilivu, na lishe duni. Umiliki salama wa ardhi huwezesha uwekezaji endelevu na kuleta tofauti kati ya kulima ili kusogeza siku na kulima kwa ajili ya kupata uhakika wa chakula wa muda mrefu.”

Ili kukabiliana na changamoto hizi, ripoti inashauri kuwepo kwa utashi wa kisiasa wa kuimarisha usalama wa milki za ardhi, hasa kwa jamii za asili na wafugaji. Sélim Louafi kutoka kituo cha utafiti cha CIRAD amebainisha kuwa ushahidi uliokusanywa ni msingi wa kutengeneza sera jumuishi na za haki kitaifa na kimataifa.

Hatua za haraka zinahitajika ili kulinda asilimia 40 ya misitu ambayo bado iko hatarini kutokana na kukosa utambuzi wa kisheria, jambo ambalo ni muhimu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na hifadhi ya mazingira.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *