
Kibaha. Wanafunzi wa sekondari katika kata za Mtambani na Janga, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani, wanatarajiwa kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata masomo, kufuatia mpango wa ujenzi wa shule mpya unaosukumwa na mbunge wa jimbo hilo.
Akizungumza Februari 25, 2026 katika kikao cha kwanza baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025 kilichowakutanisha viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya matawi na kata mjini Mlandizi, mbunge huyo amesema tayari Sh700 milioni zimetengwa kujenga shule ya sekondari Mtambani, huku Sh500 milioni zikitengwa na Halmashauri ya Kibaha Vijijini kwa ajili ya shule ya sekondari Janga.
Amesema lengo ni kupunguza umbali wanaotembea wanafunzi, ambapo wa Janga husafiri zaidi ya kilomita saba kwenda shule za Dosa Azizi na Mihande, na wa Mtambani zaidi ya kilomita tano kwenda Sekondari ya Kilangalanga.
Mbunge huyo amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa viongozi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa bila migawanyiko, akiahidi kufanya kazi na kila kiongozi kwa manufaa ya wananchi.
Kwa upande wao, viongozi wa CCM wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wilaya, Mkali Kanuso, wamemshukuru mbunge huyo kwa kuitisha kikao hicho na kuahidi kuimarisha umoja ili kusukuma mbele maendeleo ya jimbo.