
Shirika lisilo la Kiserikali (NGO) Marekani National Endowment for Democracy (NED), ambalo lilianzishwa na shirika kuu la kijasusi nchini humo, CIA, limekiri kuwa lilitumia takriban vifaa 200 vya Starlink nchini Iran wakati wa machafuko ya hivi karibuni.
Kauli hiyo ilitolewa na rais wa NED, Damon Wilson, wakati wa kikao cha kusikilizwa katika Bunge la Marekani, kabla ya wabunge kumkatiza na kusema kuwa mada hiyo haipaswi kujadiliwa hadharani.
Wilson alisema siku ya Jumanne kuwa NED “ilianza kusaidia kupeleka na kuendesha takriban vifaa 200 vya Starlink mapema” wakati wa machafuko hayo. Hata hivyo, Mbunge Lois Frankel alimkatiza na kusema: “Unajua nini, nitakukatiza—ni bora tusizungumzie hilo.”
NED, shirika ambalo lilianzishwa na CIA lakini hujieleza kama shirika linalosaidia harakati za kisiasa na kijamii nje ya Marekani, pia limekiri kushiriki katika kuunda mwelekeo wa taarifa za vyombo vya habari kuhusu kifo cha Mahsa Amini mjini Tehran mnamo Septemba 2022, tukio lililosababisha machafuko yaliyoelezwa ambayo, wakuu wa Iran walisema yalichochewa kutoka nje ya nchi.
Amini alikuwa mwanamke Muirani aliyefariki hospitalini siku kadhaa baada ya kuanguka katika kituo cha polisi mjini Tehran. Baada ya kifo chake, machafuko yaliibuka katika miji kadhaa ya Iran.
Wilson amesema washirika wa NED walihusika katika kueneza taarifa kuhusu tukio hilo ambazo zilikuwa za upotoshaji.
Aidha amesema NED ilikuwa muhusika muhimu katika machafuko ya hivi karibuni nchini Iran, ambapo waandamanaji wenye silaha walivamia miji kadhaa, wakaua polisi na raia, na kuchoma misikiti pamoja na mali za umma na binafsi.
Rais huyo wa NED aliendelea kueleza ushirikiano wa shirika hilo na NGO na mitandao ya vyombo vya habari, akisema kuwa walikuza simulizi zinazolaumu serikali ya Iran kwa kile walichokiita usimamizi mbaya wa rasilimali, ikiwemo maji katika mji wa Tehran.
Maandamano yaliyozuka mwanzoni mwa Januari 2026 yalianza kwa amani yakilenga malalamiko ya kiuchumi, ikiwemo kushuka kwa thamani ya sarafu, lakini baadaye yaligeuka kuwa machafuko ya vurugu baada ya kuingiliwa magenge ya wahalifu waliounga mkono na tawala za kigeni
Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi wa Iran, Ahmad‑Reza Radan, baadhi ya waliokamatwa walikiri kupokea malipo kwa sarafu ya dola kutoka nje ya nchi na kubeba silaha pamoja na vilipuzi kwa ajili ya kushambulia malengo yao.
Ripoti zinaonesha kuwa wapiganaji wanaohusishwa na Mossad ya Israel, pamoja na makundi ya kujitenga yenye makao yao kaskazini mwa Iraq, waliingia kwa siri katika maandamano ya awali ya amani, wakilenga majengo ya serikali, vituo vya polisi, masoko, na maeneo ya kidini.
Machafuko hayo yalisababisha uharibifu wa mamia ya misikiti, ofisi za serikali, na miundombinu mingine ya umma.