Rais wa Marekani Donald Trump amekoleza maradufu moto wa kampeni yake ya kueneza sumu dhidi ya Iran kwa kurudia tena tuhuma hewa za kila mara kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.
Kwa mujibu wa Pars Today, Trump amerudia tena madai na kauli zake zinazokinzana, akidai kwamba ‘Iran inataka zaidi kufikia makubaliano kuliko mimi’. Katika mkutano na wanahabari, rais wa Marekani amesema: “Iran inataka zaidi kufikia makubaliano kuliko mimi, lakini haiko tayari kutamka haya ‘maneno ya mazingaombwe’ kwamba haitaunda bomu”. Trump amesema: “Mazungumzo muhimu yatafanyika Geneva Alkhamisi. Iran inataka sana kufikia makubaliano, lakini haiwezi kutamka ibara, ‘Hatutaunda silaha ya nyuklia.'”
Siku ya Jumanne, Februari 24, wakati Trump alipotoa hotuba yake ya kila mwaka kwa taifa mbele ya Bunge la Marekani, alidai: “kipaumbele changu ni diplomasia, lakini sitaruhusu katu Iran iwe na silaha ya nyuklia”.
Inavyoonekana, licha ya kutuma idadi kubwa mno ya vikosi vya jeshi na zana za kivita kandokando ya Iran na kutoa vitisho mara kwa mara dhidi ya Tehran, Trump, ambaye amekabiliwa na ungangari na Muqawama wa kustaajabisha wa Iran, sasa ameamua kurudia tena tuhuma zake hewa, hususan za kudai kwamba, Iran inafanya juhudi za kumiliki silaha za nyuklia; ili kwa kufanya hivyo aeneze sumu dhidi ya Tehran, hasa za uwezekano wa Washington kuchukua hatua za kijeshi endapo mazungumzo ya sasa yasiyo ya ana kwa ana hayatofikia mwafaka.
Nukta muhimu ni kwamba, katika mgongano wa wazi unaohusiana na uchukuaji misimamo wa Marekani katika suala hilo, duru za intelijensia na ujasusi za nchi hiyo zimekiri wazi kuwa, kwa sasa, Iran haiundi silaha za nyuklia, ukiwa ni ushahidi unaopingana kikamilifu na tuhuma za mara kwa mara anazotoa Trump na maafisa wengine waandamizi wa Marekani. Katika ripoti yake kuhusu Iran iliyochapishwa Machi 25, 2025, Mkurugenzi wa Intelijensia ya Taifa ya Marekani Tulsi Gabbard alisema: “Vyombo vya intelijensia vya Marekani vingali vinaitakidi kuwa Iran haitengenezi silaha za nyuklia.”
Katika hatua inayoenda sambamba na mielekeo ya Israel na Troika ya Ulaya, Marekani imekuwa kwa miaka kadhaa ikiituhumu Iran kwamba inajishughulisha na mpango wa nyuklia wa kijeshi, licha ya kushindwa kutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha suala hilo; na kwa kutumia kisingizio hicho, imechukua hatua nyingi na kubwa za kisiasa na za uwekaji vikwazo dhidi ya Iran. Tehran kwa upande wake, imekanusha vikali tuhuma za kutaka kuunda silaha za nyuklia na kusisitiza kuwa inaendelea kuheshimu kikamilifu Mkataba wa Kuzuia Uundaji wa Silaha za nyuklia, NPT.
Iran imetangaza pia kwamba, urutubishaji wa urani hadi asilimia 60 umefanyika kama jibu tu kwa pande za Magharibi kutokana na kutotekeleza ahadi na majukumu yao kulingana na makubaliano ya JCPOA, hususan ya kuondoa vikwazo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeshasisitiza mara kadhaa kwamba, mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya amani tu, na lengo lake ni kukidhi mahitaji ya nishati na ya masuala ya tiba nchini. Kinyume na tuhuma zisizo na msingi za Magharibi kwamba Tehran ina nia ya kumiliki silaha za nyuklia, Iran imeweza kuitumia teknolojia ya nyuklia ya malengo ya amani kwa kiwango kikubwa na katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme, masuala ya tiba, kilimo, na sekta nyinginezo. Kwa kuzingatia malengo ya siku za usoni, hususan kuhusiana na mahitaji ya umeme ya Iran, uzalishaji wa umeme kwa kutumia vinu vya nyuklia umepewa mazingatio maalumu.
Sera ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebainishwa kwa uwazi na bila ya utata wowote kuwa ni ya malengo ya amani, na imejikita katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria chini ya mkataba unaopiga marufuku uundaji wa silaha za nyuklia. Sambamba na hilo, doktrini ya ulinzi ya Iran ambayo ina msingi imara wa kiitikadi na kimkakati inapiga marufuku matumizi ya aina yoyote ya silaha za maangamizi ya halaiki. Sera hii imekuwa ikisisitizwa na kuthibitishwa tena na tena na viongozi wa juu kabisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Suala jingine ambalo inapasa lizingatiwe katika muktadha huu ni kwamba, vitisho vinavyorudiwa kila mara na Marekani dhidi ya mpango wa amani wa nyuklia wa Iran vinavuka mpaka wa mzozo wa kisiasa au wa kiusalama wa baina ya pande mbili na vina taathira kubwa kwa itibari ya taasisi za kimataifa na mkataba wa kimataifa wa NPT.
Mpango wa nyuklia wa Iran unaendeshwa kwa mujibu wa mkataba unaopiga marufuku uenezaji silaha za nyuklia na kwa usimamizi kamili wa Wakala wa Kimataifa ya Nishati ya Atomiki, IAEA. Hata hivyo, Marekani na baadhi ya waitifaki wake zinautangaza mpango huo kuwa ni kitu hatari; na kwa kutumia nyenzo za kisiasa na kiuchumi, zinafanya kila njia ili kuibana Iran katika harakati yake ya kuelekea kwenye ustawi wa kisayansi na kiteknolojia. Muelekeo huo unatilia shaka kanuni ya msingi ya nchi zote kuwa na haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani.
Hayo yanajiri huku Trump akiibua tuhuma mpya dhidi ya Tehran zinazolenga kushadidisha mashinikizo na kuhalalisha hatua zake za kiuadui, ikiwemo uwezekano wa Marekani kuishambulia kijeshi Iran…/