Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, ametoa wito kwa Ukraine siku ya Jumatano wa kuwaachilia huru wafungwa wawili wa kivita wa Ghana waliopigana dhidi ya vikosi vya Ukraine katika safu ya jeshi la Urusi, wakati wa ziara ya waiziri huyo huko Kyiv.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba alikuwa na “majadiliano ya kina” wakati wa mkutano wake na waziri “kuhusu jinsi Urusi inavyowaajiri raia wa Ghana na nchi zingine za Afrika kushiriki katika vita dhidi ya Ukraine na jinsi tunavyoweza kukabiliana na hili.”

Mapema siku hiyo, Samuel Ablakwa alisema anatumai rais wa Ukraine ataonyesha “ukarimu na huruma” na kuwaachilia huru ili aweze “kurudi Ghana na Waghana hawa wawili.” Volodymyr Zelensky hakutaja kesi ya watu hawa wawili katika taarifa yake, lakini alibainisha kwamba majadiliano kuhusu suala la wapiganaji wa Afrika yataendelea kati ya nchi hizo mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiga alisema wakati wa mkutano na mwenzake wa Ghana siku ya Jumatano kwamba zaidi ya Waafrika 1,780—raia kutoka nchi 36 kote barani—walikuwa wakipigana dhidi ya Ukraine ndani ya jeshi la Urusi. Aliishutumu Moscow kwa kuwashawishi watu hawa kujiunga na jeshi kupitia udanganyifu na akahimiza Accra kuimarisha hatua za kuzuia Urusi kuwaajiri Waafrika. “Urusi inawaingiza Waghana ndani ya kaburi bila kujiytambua,” Sybiga alibainisha.

Wapiganaji wanadanganywa kwenda Urusi

Mwenzake wa Ghana alidai kwamba Waafrika wanaojiunga na jeshi la Urusi “hawakuamriwa na serikali za Afrika.” Waghana walioenda vitani “ni waathiriwa wa udanganyifu na taarifa potofu” na “mitandao ya wafanyabiashara haramu ya wahalifu” ambayo inawaahidi “kazi nzuri” nchini Urusi, alisema. “Hawana historia ya usalama, hawana historia ya kijeshi. Hawajafunzwa, na walivutiwa tu, kisha wakadanganywa na kupelekwa kwenye mstari wa mbele kwenye uwanja wa vita,” alisema Samuel Ablakwa.

Aliishukuru Ukraine kwa “kuheshimu sheria ya kimataifa” katika kuwatendea vizuri wafungwa wa kivita wa Ghana. “Tumepokea ripoti zinazoonyesha kwamba wako katika afya njema,” alisema, kabla ya kuongeza: “Hawajateswa. Hawajapata mateso yoyote ya kinyama tangu walipokamatwa.”

Katika miezi ya hivi karibuni, nchi kadhaa za Afrika, hasa Kenya na Uganda, zimeanza kujua hatima ya raia wao walioajiriwa katika jeshi la Urusi, ambao mara nyingi huishia kuuawa au kukamatwa nchini Ukraine. Wakenya kadhaa waliohojiwa na shirika la habari la AFP baada ya kufanikiwa kurudi nyumbani walisimulia kukutana na Waafrika kadhaa katika kambi za mafunzo nchini Urusi au kwenye mstari wa mbele, wakitoka Nigeria, Cameroon, Misri, na Afrika Kusini. Watu hawa walisema kwamba walishawishiwa na ahadi za kazi za kiraia zenye malipo mazuri nchini Urusi, kabla ya kulazimishwa kujiunga na jeshi la Urusi na kutumwa kupigana nchini Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *