
Watu wanne waliokuwa ndani ya boti iliyosajiliwa Florida waliuawa na wengine sita kujeruhiwa siku ya Jumatano, Februari 25, na walinzi wa mpaka wa Cuba baada ya makabiliano katika maji ya eneo la Cuba, Wizara ya Mambo ya Ndani imetangaza katika taarifa. Cuba imelaani tukio hilo kama jaribio la kundi lenye silaha “kuingia ” nchini humo kwa “malengo ya kigaidi.” Kwa upande wake mahakama ya Florida imetangaza kuwa imefungua uchunguzi.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Imebainika kuwa boti hiyo ya mwendo kasi iliyoangamizwa, ambayo ilisajiliwa Florida chini ya nambari FL7726SH, ilikuwa imebeba watu 10 wenye silaha ambao, kulingana na taarifa za awali kutoka kwa wafungwa, walikusudia kuingia nchini kwa malengo ya kigaidi,” Wizara ya Mambo ya Ndani imesema katika taarifa kwa vyombo vya habari. “Bunduki za kivita, silaha nzito nzito, vilipuzi vilivyotengenezwa kienyeji, fulana zisizopitisha risasi, kofia zenye miwani hatari ya kivita, na sare za kujificha msituni zilikamatwa,” taarifa hiyo imeongeza.
“Kufuatia makabiliano hayo […], washambuliaji wanne kutoka upande wa kigeni waliuawa na sita walijeruhiwa, ambao walihamishwa na kupokea msaada wa kimatibabu,” taarifa ya awali kutoka kwa mamlaka ya Cuba ilibainisha, bila kutaja uraia wa wale waliouawa au kujeruhiwa.
Wakati wa tukio hilo, lililotokea muktadha wa mvutano mkubwa kati ya Cuba na Marekani, nahodha wa chombo hicho cha Cuba, ambacho walinzi watano wa mpaka walikuwa wakihudumu, pia alijeruhiwa, kulingana na chanzo hicho.
Kulingana na taarifa hiyo, “asubuhi ya Februari 25, 2026, boti ya mwendo kasi iliyosajiliwa Florida, nchini Marekani, chini ya nambari FL7726SH, iligunduliwa katika maji ya eneo la Cuba,” katika eneo la mfereji wa El Pino, katika jimbo la Villa Clara (katikati mwa Cuba).
Risasi zilirushwa kutoka kwa chombo kilichosajiliwa Florida
Wakati chombo cha doria cha mpakani “kilipokaribia kukitambua, risasi zilirushwa kutoka kwa boti ya mwendo kasi kwa wanajeshi wa Cuba,” taarifa hiyo inaelezea. Wizara ya Mambo ya Ndani inabainisha kwamba inaendelea na uchunguzi wake “ili kufafanua ukweli kikamilifu.”
Serikali ya Cuba mara kwa mara huripoti uvamizi wa boti za mwendo kasi kutoka Marekani katika maji ya eneo lake, kwa ujumla zikihusishwa na biashara haramu ya binadamu, zikihusisha makundi ya wahamiaji wanaotaka kuondoka kisiwani humo, au biashara haramu ya dawa za kulevya.
Kulingana na taarifa za hivi punde zilizotolewa na mamlaka ya Cuba, kati ya mwezi Januari na Juni 2022, mwaka wa wimbi kubwa la uhamiaji kutoka kisiwa hiki cha kikomunisti, walinzi wa pwani walizikamata boti kumi na tatu za mwendo kasi kutoka Marekani kuhusiana na “shughuli za biashara haramu ya binadamu kutoka Cuba hadi nchi hiyo.”
Mwaka huo, boti ya mwendo kasi kutoka Marekani ilifyatua risasi ilipozuiliwa na walinzi wa mpaka magharibi mwa kisiwa hicho. Mmoja wa abiria wa boti hiyo “alijeruhiwa vibaya” na risasi zilizorushwa na Walinzi wa Pwani wa Cuba wakijaribu kujihami. Baadaye alifariki kutokana na majeraha aliyoyapata.
Mwanasheria Mkuu wa Florida James Uthmeier ametangaza kufunguliwa kwa uchunguzi wa kimahakama. “Serikali ya Cuba si ya kuaminika, na tutafanya kila tuwezalo kuwawajibisha wakomunisti hawa,” aliandika kwenye mitandao ya kijamii, akiongeza kuwa ameiomba ofisi yake kufungua uchunguzi kuhusu tukio hilo.
Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance amesema Marekani ilikuwa “inafuatilia” hali hiyo. “Hii ni wazi kwamba ni hali tunayoifuatilia. Tutumaini si mbaya kama tunavyohofia, lakini siwezi kusemasana kwa sababu sijui kilichotokea,” amewaambia waandishi wa habari. Vance ameongeza kuwa Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, ambaye anahudhuria mkutano wa kilele huko Karibiani, alimpa taarifa mapema, lakini kwamba “hawakuwa na maelezo mengi.”
Rubio atoa wito wa “mabadiliko makubwa” nchini Cuba
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kwamba Washington ingejibu “ipasavyo.” “Tunapokusanya taarifa zaidi, tutakuwa tayari kujibu ipasavyo,” alibainisha.
“Cuba lazima ibadilike kwa kiasi kikubwa kwa sababu ndiyo nafasi yake pekee ya kuboresha ubora wa maisha kwa watu wake … Ikiwa wanataka kutekeleza mageuzi haya makubwa ambayo yanafungua njia ya kiuchumi na, hatimaye, uhuru wa kisiasa kwa watu wa Cuba, ni wazi kwamba Marekani ingefurahi kuona hilo,” alitangaza. Aliongeza kwamba “watu wa Cuba wameteseka kwa muda mrefu” na kwamba “mamlaka na serikali wanawajibika kwa hili.”