
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewaalika wawekezaji kutoka Ufaransa kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali za uchumi visiwani humo hasa sekta ya utalii na kusema kuwa Zanzibar iko tayari kupokea uwekezaji wenye tija na endelevu.
Rais Mwinyi ametoa wito huo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Anne Sophie katika mazungumzo yaliyolenga kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kiuchumi. SOMA: Rais Mwinyi ataja vipaumbele 6 vya usimamizi
Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa kuboresha sera na miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara na miradi mikubwa kama Bandari Jumuishi ya Mangapwani, ambayo itakapokamilika itafungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji.


Rais Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika mkakati wa kuendeleza uchumi wa buluu pamoja na kufungua Kisiwa cha Pemba kuwa kituo cha uwekezaji na utalii endelevu hatua ambayo inalenga kuongeza ajira, utaalamu na ubora wa huduma.
Kwa upande wake, Balozi Anne Sophie amesema Ufaransa itaendelea kuunga mkono juhudi za Zanzibar katika maendeleo ya sekta muhimu zikiwemo utalii, afya, elimu, utamaduni, mazingira pamoja na uendelezaji wa Mji Mkongwe.