Mbeya. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoa wa Mbeya (Takukuru), imewarejeshea wananchi 20 wa Mtaa wa Ilomba jijini humo Sh500,000 walizochangishwa na Alex Nyagawa kwa ajili ya kuwaunganishia huduma ya umeme majumbani.

Inadaiwa kuwa, Nyagawa aliwashawishi wananchi hao wampatie fedha hizo ili awaunganishie huduma hiyo kwa bei nafuu inayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa bei ya Sh27,000 huku akijua hana uwezo wa kufanya hivyo.

Akizungumza leo  Ijumaa, Februari 27, 2026  Naibu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani humo, Jasper Luoga amesema Nyagawa alikusanya kiasi hicho cha fedha akijua hana mamlaka wala uwezo wa kufanya hivyo, na kwamba si mtumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Pia, Luoga ameongeza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa Sh107 milioni kati ya Sh125 milioni ambazo hazikuwasilishwa kwenye akaunti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali baada ya mapato hayo kukusanywa na watoza ushuru.

“Kwa maana hiyo kila mwananchi amerejeshewa Sh25,000 ambazo walichanga kwa mwananchi huyo ili kuwaunganishia huduma ya umeme kwa bei nafuu inayotolewa na REA,” amesema Luoga.

Mkuu huyo ameongeza kuwa kwa kipindi cha miezi mitatu (Oktoba hadi Desemba), Takukuru ilifanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo 29 ya zaidi ya Sh12 bilioni na kushauri upungufu kurekebishwa ili kuendana na thamani ya fedha hizo.

Pia, ameeleza kuwa, taasisi hiyo ilifanya uchambuzi wa mifumo ya utoaji huduma (FFARS), sekta ya afya unaowezesha udhibiti wa matumizi yasiyofaa ya fedha kwenye vituo vya afya.

“Kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu, tumejipanga kutoa elimu kwa wanafunzi, wananchi na watumishi wa umma juu ya athari za rushwa, kuendelea kufuatilia matumizi sahihi ya fedha za miradi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaohusika na vitendo vya rushwa,” amesema Luoga.

Amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo akieleza kuwa, kwa kufanya hivyo itasaidia uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za umma kwa manufaa ya Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *