
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesisitiza kwamba, mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu na Marekani yatafanikiwa tu iwapo Washington itayachukuliwa kwa uzito na kuzingatia uhalisia wa mambo.
Katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri, Badr Abdelatty jana Ijumaa, Araghchi aliashiria maendeleo ya hivi karibuni katika mazungumzo ya Iran na Marekani, hasa duru ya tatu iliyofanyika Geneva siku ya Alkhamisi na kusisitiza kujitolea kwa Tehran kutumia diplomasia kutatua masuala yenye utata.
Araghchi amesisitiza kwamba, “Mafanikio katika njia hii yanahitaji uzingatiaji na uhalisia kutoka kwa upande wa pili (Marekani) na kujiepusha (kwake) na hesabu yoyote isiyo sahihi, na kujipendea makuu.”
Kwa upande wake, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri amesisitiza uungaji mkono wa nchi yake kwa juhudi za kidiplomasia zinazolenga kutatua masuala yaliyosalia kuhusu mradi wa nyuklia wenye malengo ya amani wa Iran.
Amesisitizia haja ya mazungumzo kati ya Tehran na Washington kuendelea ili kufikia suluhisho “la wastani” ili kuzuiakuongezeka kwa taharuki katika eneo la Asia Magharibi. Abdelatty pia amebainisha kuwa, suluhisho lolote la kijeshi litakuwa na matokeo mabaya sana katika eneo hili lote.
Kadhalika, Waziri Araghchi hiyo jana alifanya mazungumzo ya simu na mwenzake wa Iraq Fuad Hussein, ambapo walijadili masuala ya kimataifa na kikanda, yakiwemo mazungumzo ya nyuklia.
Katika mazungumzo ya simu na Hussein, mwanadiplomasia mkuu wa Iran aliashiria umuhimu wa kudumisha mazungumzo kati ya nchi za kikanda ili kulinda amani na utulivu wa eneo hili.