Kamati ya Utendaji ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imeonyesha wasiwasi wake kuhusu vitisho vya hivi karibuni dhidi ya Iran.

Katika mkutano wa dharura uliofanyika mjini Jeddah nchini Saudi Arabia, nchi wanachama wa OIC zimetangaza kuwa na wasiwasi kuhusu vitisho dhidi ya mamlaka ya kujitawala ya Iran na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za kidiplomasia.

Marekani imekuwa ikitishia kuishambulia Iran kijeshi iwapo pande mbili hizo hazitafikia makubaliano katika mazungumzo yanayoendelea yasiyo ya moja kwa moja baina ya pande mbili. Jumuiya ya OIC imekaribisha juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia kati ya Iran na Marekani, ikisisitiza haja ya kuchukuliwa hatua za kujenga ili kupunguza mvutano.

OIC imesema inatambua na kupongeza juhudi zilizofanywa na nchi kama Oman, Uturuki, Qatar, Misri, na Saudi Arabia katika kufanikisha mazungumzo haya.

Wakati huo huo, Samir Bakr Dhiab, Naibu Katibu Mkuu wa OIC kwa Palestina na Al-Quds amebainisha hatari zinazotokana na mienendo ya utawala wa Israel, akisisitiza, Israel haina mamlaka juu ya eneo lolote la Palestina, kama vile Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na mji mtakatifu wa Al-Quds.”

Kamati ya Utendaji ya OIC imelaani sera za makazi ya utawala wa Israel katika Ukingo wa Magharibi na kutaja matumizi yoyote ya nguvu dhidi ya taifa huru kama ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa.

Mnamo Februari 8, serikali ya Israel iliidhinisha maamuzi kadhaa yaliyolenga kufanya mabadiliko katika hali ya kisheria na kiraia katika Ukingo wa Magharibi, kwa lengo la kuimarisha udhibiti wake wa maeneo hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *