DAR ES SALAAM: MWANAMITINDO nguli wa Kimataifa Mtanzania anayeishi nchini Ufaransa, Miriam Odemba, ametunukiwa tuzo ya heshima na Uongozi wa Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu iliyopo Temeke Dar es Salaam kwa kutambua mchango wake shuleni hapo.
Miriam Odemba ametunukiwa tuzo hiyo katika siku yake ya kuzaliwa iliyoambatana na utoaji misaada, chakula cha pamoja na viongozi wa taasisi yake ya Miriam Odemba Foundation shuleni hapo.

Imekuwa desturi ya mwanamitindo huyo kutoa misaada, kujumuika na watoto wenye uhitaji kwenye vituo mbalimbali vya mahitaji maalumu nchini kupitia taasisi hiyo.
Akizungumza na Dailynews, mara baada ya kutolewa tuzo hiyo, Miriam Odemba alisema haoni kuwa yeye ni bora zaidi ya wengine bali ni mwanamke mwenye deni la kuendelea kurudisha kwa jamii inayompenda kwa dhati, jamii inayoishi kwa uhitaji, na makundi maalumu.
“Hii ni jamii ya watu wenye moyo kama wangu, ndoto kama zangu, na furaha kama yangu, wanacheka, wanahisia, wana imani na pia wana uthubutu kama wangu,” alisema Miriam Odemba.

Alisema furaha yake ni kuona watoto wanakula, wanavaa, wanacheza na kujifunza pia, ili waendelee kutimiza ndoto zao, malengo na kujiamini katika ukuaji wao.
Aliwapa moyo kwa kusema kuwa kuwa mlemavu haizuii kufanikiwa kuwa na furaha, wala kuwa na bidii. Alieleza kuwa kipimo cha yote ni ndani ya nafsi na mioyo.

Aidha, akizungumza taasisi yake, Miriam alisema lengo la kuanzisha taasisi hiyo ni kuleta mabadiliko chanya kwa jamii, kwani hadi sasa wamefanikisha ujenzi wa madarasa, visima, na kushiriki moja kwa moja kugusa maisha ya mwanamke, watoto hasa mabinti.
Alisema wamefanikiwa kuhudumia mabinti kwenye kampeni zao mbalimbali, kuinua elimu, vipaji, kufundisha maadili, kuhamasisha maendeleo ya afya ya mwili na akili.

“Tangu kuanzishwa kwa taasisi imekuwa njia ya kufanya kazi mbalimbali za kijamii, huku ikishuhudiwa jinsi mwanzilishi anavyopenda kucheza na watoto, kucheka nao na kuwahudumia mahitaji mbalimbali,” alisema Miriam.
Miriam Odemba alisema kituo hicho kimekuwa kituo mama kwake kila anapokuwa nyumbani, iwe likizo au kwenye majukumu mengine, amekuwa akiwatembelea karibia kila mwaka.

“Furaha hii ya Miriam Odemba kusherehekea siku ya kuzaliwa ni ishara ya upendo wa dhati kwa jamii nzima ya kitanzania hasa wale wenye uhitaji, ikiwemo walio kwenye makundi maalumu,”
Alisema kuwa ataendelea kuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wengine kuwa na moyo kama wake na zaidi, na kuijenga jamii bora, kuliko zote, zenye utu, asili na hadhi halisi ya kiafrika.
Novemba 28, 2021, Miriam Odemba kupitia taasisi yake alifika kutoa msaada kwa watoto wenye uhitaji katika kituo cha watoto yatima cha Salvation Army kilichopo Temeke. Pamoja na zawadi mbalimbali, Miriam pia alipata chakula cha pamoja na watoto hao.

Sio hivyo tu, Agosti 30, 2019, akiwa na taasisi yake, Odemba alifika wilayani Mkuranga mkoani Pwani kuzungumza na wanawake wajasiriamali kuona namna ya kuwasaidia masuala mbalimbali ikiwemo changamoto ya maji waliyokuwa wakipitia kipindi hicho.
Katika safari hiyo, Odemba alichangia Dola 10,000 kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuongeza maji ambao unaendelea kusaidia wakazi wa eneo hilo hadi sasa.

Imekuwa ni desturi ya mwanamitindo huyo kwani aliwahi pia kutembelea Shule ya Msingi Mwongozo Katika ziara yake shuleni hapo, aliyoifanya Oktoba 9, 2019, Wilaya ya Mkuranga, Odemba na taasisi yake alifanikisha ujenzi wa baadhi ya madarasa baada ya kuona idadi kubwa ya wanafunzi huku madarasa yakiwa machache.
Desemba 10, 2019 Wiki ya Maadhimisho Haki za Binadamu, MOF ilifika maeneo mbalimbali ya vijijini kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wanafunzi wa shule za msingi. Hatua hii imekuwa endelevu kwa taasisi hiyo kufika maeneo ya vijijini kutoa huduma ya maji safi kwenye maeneo mengi nchini.

Februari 19, 2025 katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa ya uongozi wa taasisi MOF ilisherehekea siku hiyo pamoja na wanafunzi wa Dar es Salaam Girls Secondary School kwa kukata keki, kutoa zawadi mbalimbali, kutoa elimu na kuwahamasisha mabinti kupambania ndoto zao bila kukata tamaa.
Pamoja na kutoa misaada mbalimbali kwenye maeneo tofauti, Taasisi ya Miriam Odemba foundation ilikabidhiwa cheti cha utambulisho na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) kama ishara ya shukrani kwa mchango wao bora katika sanaa na utamaduni wa Tanzania.

“Tunafurahia ushirikiano wetu na fursa nzuri ambazo ziko mbele yetu tunaposhirikiana kuleta mabadiliko ya kipekee,” inaaleza taarifa ya MOF.
MOF ni taasisi isiyo ya kiserikali iliyowekeza kusaidia mabinti, watoto na vijana nchini Tanzania, iliyoanzishwa na mwanamitindo Mtanzania Miriam Odemba, anayeishi UfaransaTaasisi ya MOF, imejikita kutafuta suluhisho endelevu la changamoto zinazowakabili wanawake na watoto barani Afrika, hasa nchini Tanzania.