Unguja. Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imemalizia kazi ya kuteketeza nyaraka 720,000 za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025.
Kati ya nyaraka hizo 100,000 hazikutumika, zilizotumika Unguja ni nyaraka za kura 461,000 na Pemba kura 159,000.
Akizungumza wakati wa kuteketeza nyaraka hizo leo Jumamosi, Februari 28, 2026 katika Shimo la Muungoni Mkoa wa Kusini Unguja, Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji George Joseph Kazi amesema wametekeleza hayo kwa mujibu wa matakwa ya sheria baada ya kutopokea zuio lolote la Mahakama.
“Sheria ya Uchaguzi ya Mwaka 2018 inaeleza kwamba, siku 90 baada ya uchaguzi mkuu ZEC inapaswa kuziteketeza nyaraka kama kutakuwa hakuna amri yoyote ya Mahakama kuzuia uteketezaji huo,” amesema Jaji Kazi.
Maofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, wakiteketeza nyaraka zilizotumika wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 katika shimo la Muungoni Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Shughuli ya uteketezaji wa nyaraka hizo ilianza Februari 18, 2026 Pemba baada ya siku 90 kutokana na kwamba kulikuwa hakuna zuio lolote la kimahakama la kufanya tume isiweze kutekeleza nyaraka hizo.
Akizungumzia kuwapo kesi mahakamani kuhusu masuala hayo ya uchaguzi, Jaji Kazi amesema kuwepo kwa kesi ni suala moja na kuwepo kwa zuio ni suala jingine.
“Ni kweli zipo kesi za uchaguzi kwa upande wa Unguja lakini kwa Pemba tayari zimeshatupiliwa mbali kutokana na kasoro mbalimbali za watu waliopeleka maombi,”amesema.
“Kwa Unguja zipo ambazo zimeshasikilizwa lakini nyingine bado hazijasikilizwa lakini zilifunguliwa bila ya kuwepo ombi lolote la Mahakama la kuzuia uteketezaji wa nyaraka na ZEC haikupokea amri yoyote kutoka mahakamani ya kuweza kuzuia utekelezaji wa sheria,” amesema.
Maofisa wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar ZEC, wakiteketeza nyaraka zilizotumika wakati wa uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025 katika shimo la Muungoni Mkoa wa Kusini Unguja. Picha na Jesse Mikofu
Jaji Kazi amesema tume inafuata sheria na mtu yeyote ambaye anaona wanakwenda kinyume na sheria basi anaweza kwenda kushitaki mahakamani na Mahakama ndio itaona iwapo kuna ukiukwaji wa sheria.
“Kama Mahakama ikihitaji tutaeleza kwamba sheria inavyosema siku ni 90 na ingeweza kuweka zuio na sisi tumefuata matakwa ya sheria,” amesisitiza.
Mkuu wa Divishion ya Tathmini na Uhamishaji Nyaraka kutoka Taasisi ya Nyaraka Zanzibar, Zuwena Rajab Ali amesema kwa mujibu wa sheria ya nyaraka ya mwaka 2008 kifungu cha 13 mpaka 15 kinawapa mamlaka ya kusimamia kazi ya uteketezaji wa nyaraka.
“Sheria ya nyaraka inasema kwamba, hizo ni kumbukumbu kwani nyaraka huwezi kuiteketeza, kumbukumbu zina kiwango chake na muda wake ukifika kwa mujibu wa thamani ambayo ilikuwa nayo inaweza kuteketezwa kwani hazina thamani tena,”amesema.
Amebainisha kwamba, taasisi yao haihifadhi kumbukumbu hiyo ya karatasi kwa ajili ya miaka ya mbele bali wanachohifadhi ni matokeo ya uchaguzi.
“Kwa sababu karatasi hizi utazihifadhi kwa miaka mingapi na zitakaa wapi lakini matokeo ni muhimu na yeyote anayekuja anayehitaji basi anapatiwa, kwani tangu miaka ya nyuma kabla ya mapinduzi, ukija kwenye taasisi yetu tunayo matokeo ya chaguzi ambazo zimefanyika,” amesema.
Sheha wa Shehia ya Muugoni, Mussa Juma Mbwato amesema Serikali ya kijiji ilipata taarifa ya kazi hiyo na kuliridhia.