
Dar es Salaam. Watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakabiliwa na hatari kubwa ya kuugua kutokana na matumizi ya chakula kisicho salama, huku wakikumbwa na magonjwa hayo kwa kiwango karibu mara tatu zaidi ya watoto wakubwa na watu wazima, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeeleza.
Makadirio mapya ya shirika hilo yanaonyesha kuwa licha ya watoto hao kuwa asilimia tisa pekee ya idadi ya watu duniani, wanachangia karibu theluthi moja ya visa vyote vya magonjwa yatokanayo na chakula kisicho salama.
Magonjwa ya kuharisha yanaendelea kuwa tishio kubwa kwa kundi hilo, huku kemikali hatari kama risasi (lead) na methylmercury zinazoweza kupatikana katika vyakula vikitajwa kusababisha madhara ya kudumu katika ukuaji wa ubongo na mfumo wa fahamu wa watoto.
WHO inakadiria kila mwaka watu 866 milioni huugua kutokana na chakula kisicho salama na wengine milioni 1.5 hufariki dunia.
Sehemu kubwa ya madhara hayo, kwa mujibu wa shirika hilo, yanaweza kuzuilika kupitia upatikanaji wa maji safi, usafi wa mazingira, uhifadhi bora wa chakula na huduma za afya.
Akizungumzia hilo daktari bingwa wa afya ya jamii, John Msuya, amesema watoto wadogo wako katika hatari zaidi kwa sababu kinga zao za mwili bado hazijakomaa vya kutosha kupambana na vimelea vinavyopatikana kwenye chakula.
“Mtoto anapopata maambukizi ya mara kwa mara ya kuhara au magonjwa mengine yanayotokana na chakula, sio tu kwamba afya yake huathirika kwa wakati huo, bali hata ukuaji wake wa mwili na uwezo wa kujifunza baadaye unaweza kuathirika,” amesema Dk Msuya.
Amesema changamoto kubwa katika nchi nyingi zinazoendelea ni ukosefu wa mifumo madhubuti ya kuhakikisha usalama wa chakula kuanzia shambani, sokoni hadi mezani kwa mlaji.
Kwa mujibu wa WHO, Afrika na Kusini-Mashariki mwa Asia zinaendelea kubeba mzigo mkubwa zaidi wa magonjwa yatokanayo na chakula, zikichangia karibu robo tatu ya magonjwa yatokanayo na chakula duniani na asilimia 60 ya vifo vyake.
Ripoti hiyo inaonyesha vimelea vya kibaiolojia kama bakteria, virusi na vimelea wengine vilisababisha zaidi ya visa milioni 860 vya magonjwa yanayotokana na chakula mwaka 2021.
Hata hivyo, kemikali mbalimbali zilichangia asilimia 73 ya vifo vyote vilivyohusishwa na chakula kilichochafuliwa.
Miongoni mwa kemikali hizo ni zile zinazohusishwa na magonjwa ya moyo, saratani na matatizo mengine ya muda mrefu ya kiafya.
Mtaalamu wa lishe na afya ya watoto, Neema Mhando, amesema athari za kemikali hizo mara nyingi hazionekani haraka kama ilivyo kwa magonjwa ya kuambukiza, jambo linalofanya watu wengi kupuuza hatari yake.
“Mtoto anaweza kula chakula chenye kiwango kidogo cha kemikali hizi kwa muda mrefu bila dalili za haraka kuonekana. Lakini baadaye tunaweza kuona matatizo ya ukuaji wa akili, uwezo mdogo wa kujifunza au changamoto nyingine za kiafya zinazodumu maisha yote,” amesema Neema.
Neema amebainisha kuimarisha usalama wa chakula kuanzia uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi hadi matumizi ya mwisho ni hatua muhimu ya kulinda afya za watoto na kupunguza mzigo wa magonjwa yanayoweza kuzuilika.
“Kuchelewa kuchukua hatua kunamaanisha kupoteza maisha zaidi na kuongeza gharama za matibabu. Huu ni wakati wa kuwekeza katika mifumo ya usalama wa chakula na elimu kwa jamii,” amesema Neema.
Mbali na madhara ya kiafya, WHO inakadiria kuwa magonjwa yatokanayo na chakula kisicho salama yalisababisha hasara ya dola za Marekani 310 bilioni kutokana na kupungua kwa uzalishaji wa kiuchumi mwaka 2021.
Kiwango hicho huongezeka hadi dola 647 bilioni kinapopimwa kwa kuzingatia tofauti za gharama za maisha kati ya nchi mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema usalama wa chakula linagusa maisha ya kila siku ya watu wote duniani.
“Kwa mara ya kwanza nchi zina takwimu zinazozionesha maeneo yenye mzigo mkubwa zaidi wa magonjwa haya, jambo litakalosaidia kupanga mikakati ya kuwalinda wananchi,” amesema Dk Tedros.
WHO imeeleza kuwa kemikali nyingi huingia kwenye mnyororo wa chakula kupitia shughuli za kilimo, viwanda na uchafuzi wa mazingira.
Shirika hilo linazitaka serikali kuimarisha udhibiti wa matumizi ya kemikali, usimamizi wa viwanda na mifumo ya ufuatiliaji wa ubora wa chakula.
Kwa upande wake, mtaalamu mazingira Salum Mwakyusa, amesema athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongeza hatari ya uchafuzi wa chakula kutokana na kuongezeka kwa joto na mabadiliko ya mifumo ya uzalishaji wa chakula.
“Kadri joto linavyoongezeka ndivyo baadhi ya bakteria na vimelea vinavyosababisha magonjwa vinavyopata mazingira bora zaidi ya kustawi. Hii ina maana kuwa usalama wa chakula sasa si suala la afya pekee bali pia la mazingira na maendeleo,” amesema Mwakyusa.