Rungwe. Wakulima wa Parachichi Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya wameomba Wakala wa Vipimo (WMA), mkoani hapa kuingilia kati na kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kubaini uchakachuzi wa mizani ya kidigitali kutumika kuwaibia.

Hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya muda mrefu ya wakulima hususani maeneo ya vijijiji kudai wanunuzi kutumia mizani iliyo nembo za mamlaka husika na kuzichakachua kama njia ya kupunguza uzito wa zao hilo.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Wakulima (Wandiru Amcos), Lusekelo Mwakibete, leo Jumamosi Februari 28,2026 kwenye mkutano wa wadau na wakulima wa Parachichi Wilaya ya Rungwe mkoani hapa.

Mkutano huo umeitishwa na WMA Mbeya kutoa elimu ya umuhimu wa uhakiki wa nembo kwenye mizani pindi wauzapo mazao sambamba kusikiliza malalamiko ya wakulima.

Muonekano wa mizani ya kidigitali inayotakiwa kutumiwa na wakulima kupima mazao hususani parachichi kuingiza sokoni. Picha na Hawa Mathias

“Mimi ni mstaafu pensheni yangu nimekuja kuwekeza kwenye kilimo cha parachichi, lakini wanunuzi hawataki kutumia mizani sahihi tunaomba ufanyike ukaguzi wa kushtukiza ili kutuokoa wakulima wanyonge, “amesema.

Mwakibete amesema asilimia kubwa parachichi ni zao la kimkakati na kuchangia mapato ya halmashauri, lakini wapo watu wachache wanajinufaika na jasho walilo tumia wakulima kuzalisha.

“Jambo lingine wanunuzi wanachezesha mizani chini ya eneo la kasha la kupimia parachichi na kusababisha kupunguza kilo moja hadi mbili hali ambayo imekuwa ikiwanyonya wakulima kushindwa kunufaika,”amesema.

“WMA, tunaomba tusaidieni wakulima nendeni fanyeni kaguzi hususani mashambani ili kuwabaini kilio hiki cha wakulima na kuweza kunusuru mapato yanayo potea na kunufaika watu wachache,” amsema.

Meneja wa WMA, Mkoa wa Mbeya,  Hassan Mrisho amesema suala hilo watalifanyia kazi haraka na kuwataka wakulima kuzingatia kuangalia nembo ya wakala wa vipimo kwenye mizani kabla ya kupima mazao.

“Mizani ilizohakikiwa tumeweka nembo ya wakala wa vipimo ,lakini kuhusu ombi la ukaguzi tunafanya kila mwaka kuona matumizi sahihi ya mizani kupimia mazao na tutaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza,”amesema.

Ofisa Kilimo Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Majaliwa Mwalembe amesema ukifika msimu wa mavuno kuanzia Februari hadi Machi kila mwaka kuna utaratibu wa wanunuzi kuomba vibali ambavyo uwasilisha kwa maofisa ugani maeneo husika kwa ajili ya ukaguzi wa mzani ili mkulima asiibiwe.

“Kimsingi kama idara ukibaini mnunuzi kachezesha mzani kwa lengo la kumuibia mkulima tunampa adhabu kwa kutumia sheria ndogo za halmashauri za kutozwa faini ya Sh 500,000, mpaka shilingi milioni moja au kufuta leseni na kibali cha biashara ya kununua matunda,”amesema.

Amesema katika msimu ujao kabla ya wanunuzi kuingia mashambani watafanya kikao cha wadau na wakulima kutoa elimu ili kuwasaidia wakulima kuwa salama na kuepuka kulanguliwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *