
Arusha. Methali ya siri ya mtungi aijuaye kata, inaakisi maisha ya Rose Njilo, mwanamke kutoka jamii ya kifugaji aliyepitia ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni, kisha kuamua kuwa sauti ya mabadiliko kwa wasichana na wanawake.
Rose ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mimutie Women Organization (WMO), asasi ya kiraia inayotetea haki za wanawake na wasichana katika jamii za kifugaji, ikiwamo jamii ya Kimasai.
Rose mwenye umri wa miaka 42, safari yake ya mapambano ilianza akiwa mtoto na aliozeshwa akiwa na miaka 13.
Alizaliwa na kukulia Loliondo, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha. Akiwa darasa la tano, alikatishwa masomo na kuozeshwa kwa mwanamume mkubwa kwa umri. Anasema hakujua hata maana ya ndoa, wala majukumu aliyokuwa anakwenda kuyabeba.
Kwa miaka 10 aliishi katika ndoa yenye mateso. Alipata watoto wanne wa kike, huku akikumbana na vipigo, manyanyaso na maisha ya hofu.
Mara kadhaa alijaribu kutoroka, lakini alirejeshwa. Anasimulia kuwa kulikuwa na nyakati alikata tamaa kiasi cha kutamani kujiua, lakini hakupata hata fedha ya kununua sumu.
Hatimaye, kwa msaada wa watu walioguswa na hali yake, alifanikiwa kutoroka. Baadaye alirejea kuwachukua watoto wake kabla hawajafanyiwa vitendo vya ukatili kama ukeketaji. Uzoefu huo ndio uliogeuka kuwa chanzo cha harakati zake.
Kutoka mwathirika hadi mtetezi
Baada ya kujinasua, Rose hakuishia kuokoa maisha yake pekee. Aliamua kujitoa kwa ajili ya kuwanusuru wasichana wanaokabiliwa na ndoa za utotoni, mimba za mapema na ukeketaji.
Kupitia Mimutie Women Organization, amekuwa mstari wa mbele kutoa elimu, kufichua matukio ya ukatili na kushirikiana na wadau mbalimbali kupambana na mila kandamizi.
Anasema mimba za utotoni husababisha kukatishwa ndoto, kushindwa kulea watoto vizuri na hata vifo wakati wa kujifungua.
Anasisitiza kuwa, vita dhidi ya ukatili wa kijinsia si rahisi, kwa sababu vinagusa mila na desturi zilizojengeka kwa muda mrefu.
Wapo wanaoogopa kupaza sauti kwa hofu ya kupoteza vyeo au kuonekana wamekisaliti jamii.
Kutengwa na familia
Mapambano yake hayakuwa mepesi. Baada ya kutoroka na kuanza kuikosoa wazi mifumo kandamizi, alitengwa na baadhi ya ndugu na wanajamii. Alionekana kama mtu anayekiuka mila na kuwafundisha wanawake tabia mbaya ya kupinga mateso.
Katika jamii nyingi za kifugaji, mwanamke hutarajiwa kuvumilia hadi mwisho, hata kama anapitia mateso. Kauli ya vumilia kwa ajili ya watoto imekuwa ikitumiwa kuwanyamazisha wengi.
Rose anasema ilichukua muda mrefu kwa baadhi ya ndugu kumwelewa. Hata hivyo, hakurudi nyuma. Aliamini kuwa maumivu aliyoyapitia hayapaswi kurudiwa na kizazi kingine.
Changamoto katika harakati
Akiwa mwanamke kutoka jamii ya kifugaji, amekumbana na vitisho na upinzani mkali. Wapo wanaomwona kama mtu anayeharibu ndoa au anayewazuia wazazi kupata mali kwa kuwaozesha mabinti zao mapema.
Katika baadhi ya maeneo, mtoto wa kike huonekana kama mtaji wa mifugo. Kuolewa mapema ni jambo la kawaida, hata kuanzia miaka 10 hadi 13. Aidha, kesi nyingi za ukatili hujaribiwa kumalizwa nyumbani badala ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Rose anasema jamii za kifugaji bado zinamtazama mwanamke kama mtoto asiye na sauti katika uamuzi wa familia. Hata mali inapouzwa, mara nyingi hushirikishwa wanaume pekee.
Licha ya changamoto hizo, anaendelea kushirikiana na wazee wa mila, viongozi wa Serikali na wadau wengine ili kubadilisha mtazamo huo hatua kwa hatua.
Nyumba salama kwa manusura
Mwaka 2023, Rose alianzisha nyumba salama kwa ajili ya wasichana wanaokimbia ukatili, ikiwamo wanaokataa kuozeshwa wakiwa wadogo. Kabla ya hapo, aliwahi kuwahifadhi baadhi yao nyumbani kwake, lakini aliona si salama kwa muda mrefu.
Tangu mwaka 2021 hadi sasa, wasichana 98 wamenufaika na msaada huo.
Wengi wao wameendelea na masomo kuanzia shule ya msingi hadi vyuo vya kati. Anasema elimu ndiyo silaha kubwa ya kumkomboa mtoto wa kike.
Mbali na hilo, anajivunia kushiriki kuwezesha kusimikwa kwa viongozi sita wa kimila wanawake wilayani Ngorongoro, ambao sasa wanashirikiana na wazee wa mila kutoa sauti ya wanawake katika maamuzi ya kimila.
Hatua hiyo imeanza kufungua milango ya ushiriki wa wanawake katika ngazi za uamuzi.
Ndoto ya kuona mwanamke huru
Rose anatamani kuona siku moja wanawake wa jamii za kifugaji wakiheshimika, wakitambulika na kushiriki kikamilifu katika maamuzi ya familia na jamii.
Anasema mifumo dume iliyokita mizizi kwa muda mrefu haiwezi kuvunjwa kwa siku moja, lakini mabadiliko yanawezekana kwa elimu na ushirikiano.
Anasisitiza kuwa haki ya mtoto wa kike kusoma, kuchagua maisha yake na kuishi bila hofu ni jambo lisilopaswa kujadiliwa kama hisani, bali kama haki ya msingi.
Kwa Rose, mapambano haya si kazi ya ajira bali ni wito wa maisha. Maumivu aliyopitia yamekuwa nguvu yake. Kutoka kuwa mwathirika wa ndoa za utotoni hadi kuwa mtetezi wa haki za wanawake, ameonesha kuwa hata ndani ya jamii zilizojaa vizingiti, sauti ya mabadiliko inaweza kusimama.
Ndoto yake kabla hajaondoka duniani ni kuona wasichana wa jamii za kifugaji wakiwa huru, wakisoma, wakijiamini na wakichangia maendeleo ya jamii zao bila hofu wala ukandamizaji.