Viongozi wa Iran wamelaani vikali shambulio la anga la utawala katili wa Israel dhidi ya shule ya msingi ya wasichana katika mji wa Minab, ulioko katika mkoa wa Hormozgan, kusini mwa Iran, lililopelekea kuuawa shahidi wanafunzi zaidi ya 150.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian ametoa taarifa akiomboleza “msiba huo wa kuhuzunisha” katika shule ya msingi ya Shajareh Tayyebah, na kulielezea shambulio hilo la bomu dhidi ya kituo kilichojaa wanafunzi wasio na hatia” kama “kitendo cha kikatili.”

Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, kitendo hicho cha kijinai kitakuwa sehemu isiyofutika ya historia ya uhalifu wa wavamizi dhidi ya Iran.

Taarifa hiyo ya Rais wa Iran imelaani vikali “kitendo hicho kisicho cha kibinadamu” na kutoa wito wa matibabu ya haraka na kipaumbele kwa waliojeruhiwa.

Katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi ameonya kwamba, shambulio hilo “halitakosa kujibiwa.” Amesambaza picha za kituo hicho cha elimu kilichoshambuliwa, akieleza kusikitishwa na shambulio la bomu mchana kweupe dhidi ya eneo lililojaa wanafunzi wadogo.

Kwa upande wake, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Esmaeil Baghaei amebainisha kuwa, shambulio hilo ni “kitendo dhahiri cha uchokozi na ugaidi.” Baghaei amebainisha kuwa, hujuma hiyo dhidi ya wanafunzi ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Naye Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran, Gholamhossein Mohseni-Ejei ametoa ujumbe wa rambirambi kutokana na mauaji hayo ya wasichana kadhaa wa shule katika mji wa Minab, akisisitiza kwamba bila shaka Jeshi la Iran litalipa kisasi mauaji hayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *