Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulizi haramu ya utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya vituo vyake vya anga za mbali na kuwasilisha malalamiko yake rasmi kuhusu suala hilo katika kikao cha jopo kazi la Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mashindano ya silaha katika anga za juu, ikitoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa kwa ajili ya kukabiliana na matumizi ya silaha katika anga hizo.

Mashambulizi dhidi ya miundombinu ya anga za mbali ya kiraia yanakiuka wazi Mkataba wa Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa za kibinadamu na Mkataba wa Anga za Juu, ambapo kukaa kimya mbele ya mashambulizi ya aina hiyo kunahatarisha fursa ya nchi zote kutumia kwa amani anga hizo.

Licha ya malalamiko ya Iran, lakini ni wazi kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni hazitazingatia wito unaoweza kutolewa na Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hili, kutokana na kuwa tawala mbili hizo hazizingatii hata kidogo sheria za kimataifa kutokana na ushawishi wao mkubwa na matumizi yao mabaya ya taasisi muhimu zilizopewa jukumu la kulinda amani ulimwenguni, ukiwemo Umoja wa Mataifa pamoja na Baraza lake la Usalama.

 Kwa kutilia maanani ukweli huo, Marekani na utawala haramu wa Israel zimekuwa zikikiuka hadharani sheria za kimataifa na kukandamiza mataifa mengine zikijua fika kwamba hakuna yeyote atakayeziwajibisha kisheria.  Wakati huo huo Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema kuwa mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani, yakilenga maeneo kadhaa katika mikoa ya pwani ya kusini na madaraja mawili ya kiraia katika mikoa ya mashariki kwenye njia ya reli inayoelekea katika mji mtakatifu wa Mashhad, ni uhalifu mkubwa wa kivita.

Wizara hiyo imelaani vikali mashambulizi hayo ya kichokozi yaliyofanywa na jeshi la kigaidi la Marekani mapema Alhamisi na kusisitiza azma thabiti ya taifa tukufu la Iran ya kulinda umoja wa ardhi yake, kujitawala na usalama wake wa taifa.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: ‘Mashambulizi ya kijinai ya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yaliyofanywa kwa kisingizio kisicho na msingi cha eti kujibu matukio yanayodaiwa kuhusisha meli kadhaa zilizokuwa zinapita katika Lango-Bahari la Hormuz siku ya Jumanne, sio tu ni ukiukaji wa wazi wa Kifungu cha 2 na 4 cha Hati ya Umoja wa Mataifa bali pia ni ukiukaji mkubwa wa Kifungu cha 1 na 5 cha Mkataba wa Makubaliano ya Kusitisha Vita, na ni kisingizio kinachotumiwa na Marekani kwa ajili ya kuhalalisha kuendelea kukiuka makubaliano hayo.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: Wakati ambapo taifa la Iran lenye utambuzi na ujasiri limeonyesha azimio lake thabiti la kukabiliana na maadui waovu wa Iran na kulinda mamlaka ya nchi, uhuru wa taifa, na umoja wa ardhi yake kupitia mahudhurio makubwa na yasiyo na kifani katika mazishi ya kihistoria ya kuaga mwili wa Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, utawala mbovu na wa kiwendawazimu wa Marekani, katika jaribio la kufidia kushindwa kwake kuelewa ukuu na fahari ya uzalendo wa Wairani na utiifu wao kwa maadili ya Mapinduzi ya Kiislamu, umetumia mabavu, uzushi, na uchokozi wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na kulenga njia ya reli inayoelekea Mashhad-al-Ridhaa (as). Huku ikionyesha kuchukizwa kwake na lugha chafu iliyotumiwa na rais wa Marekani pamoja na viongozi wengine wa Marekani dhidi ya taifa tukufu la Iran, Wizara ya Mambo ya Nje imesema hiyo ni dalili ya wazi ya kukiri kwao kwamba hawakuwa na nia ya kutekeleza Mkataba wa Makubaliano ya Kusitisha Vita wa tarehe 18 Juni, ikiwa ni dalili nyingine ya wazi ya nia mbaya, udhalilishaji, uchochezi wa vita, na uovu wa utawala wa Marekani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *