Mashambulizi yanayoendelea Mashariki ya Kati yanahofiwa kupandisha bei ya mafuta duniani kutokana na mataifa katika ukanda huo kuwa wazalishaji wakubwa wa mafuta, jambo litakalochochea kupungua kwa mafuta katika soko la dunia.

Marekani na Israel zilianzisha mashambulizi dhidi ya Iran jana Jumamosi, Februari 28, 2026, zikiwalenga viongozi wake na kuitumbukiza Mashariki ya Kati katika mzozo mpya ambao Rais wa Marekani, Donald Trump alisema ungeondoa tishio la kiusalama na kuwapa Waajemi fursa ya kuwaondoa watawala wao.

Mashambulizi hayo yameziweka katika taharuki nchi za Kiarabu za Ghuba zinazozalisha mafuta, huku hofu ya mzozo kupanuka ikiongezeka, na Iran ikijibu mapigo kwa kurusha makombora kuelekea Israel na mataifa mengine ya Kiarabu.

Mafuta ndiyo kipimo kikuu cha mvutano wa Mashariki ya Kati ambapo nchi hizo zinategemea uchumi wa mafuta huku zikitegewa katika kusambaza mafuta katika mataifa mengi duniani hasa Afrika.

Iran ni mzalishaji mkubwa wa mafuta na ipo mkabala na Rasi ya Uarabuni yenye utajiri wa mafuta, ikitenganishwa na mlango wa bahari wa Hormuz, ambako takribani asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta duniani hupita.

Mzozo huo unaweza kupunguza kiwango cha mafuta yanayoingia katika soko la dunia na kusababisha bei kupanda.

Kwa mujibu wa Reuters, mafuta ghafi ya Brent yalikuwa yanauzwa, Ijumaa iliyopita, kwa takribani Dola za Marekani 73 (Sh185,484) kwa pipa, yakiwa tayari yamepanda kwa takribani asilimia 20 tangu mwanzoni mwa mwaka huu.

Baadhi ya kampuni kubwa za mafuta na wafanyabiashara wakubwa walisitisha usafirishaji wa mafuta ghafi na bidhaa za mafuta kupitia mlango wa bahari wa Hormuz kutokana na mashambulizi hayo, vyanzo vinne vya biashara vilisema Jumamosi.

William Jackson, mchumi mkuu wa masoko yanayoibukia katika kampuni ya Capital Economics, alisema hata kama mzozo huo utadhibitiwa, bei ya Brent inaweza kupanda hadi takribani dola 80 (Sh203,270) kwa pipa, kiwango kilichofikiwa wakati wa vita vya siku 12 nchini Iran Juni, mwaka jana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *