
Dar es Salaam. Mijadala kuhusu tofauti kati ya wanawake na wanaume imekuwepo kwa muda mrefu, lakini mijadala inayohusu hisia na mawasiliano imekuwa nyeti zaidi kwa sababu inagusa maisha ya kila siku kama ndoa, uhusiano wa kimapenzi, familia na hata sehemu za kazi.
Mara nyingi migogoro hutokea si kwa sababu ya kukosa upendo au heshima, bali kwa sababu ya kutoelewana katika namna ya kuhisi na kuwasiliana. Waandishi na watafiti kadhaa wamejaribu kueleza tofauti hizi kwa lugha rahisi, wakisisitiza kuwa lengo si kutenganisha jinsia, bali kusaidia kujenga uelewano.
Makala hii kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya kimtandao, inaangazia tofauti hizo kwa mtazamo wa kihisia na kimawasiliano.
Namna tofauti ya kuhisi na kueleza
Mwandishi John Gray, kupitia kitabu chake: Men Are from Mars, Women Are from Venus, anaeleza kuwa wanaume na wanawake wana mifumo tofauti ya kihisia, jambo linaloathiri namna wanavyokabiliana na matatizo. Anaandika: “Wanaume na wanawake wanapaswa kuwa tofauti. Tunapokumbuka hili, uhusiano hufanya kazi.”
Kwa mujibu wa Gray, wanawake kwa kawaida huwa tayari zaidi kueleza hisia zao kwa maneno. Wanapotatizwa, wanahitaji kuzungumza ili kujisikia nafuu.
Kwa upande mwingine, wanaume wengi hujiondoa kimya kimya wanapokabiliwa na shinikizo la kihisia. Gray anafananisha hali hii na “pango” ambako mwanaume hujifungia ili kufikiri na kutafuta suluhisho.
Tatizo hutokea pale mwanamke anapochukulia ukimya huu kama kutojali, ilhali kwa mwanaume ni njia ya kujilinda kihisia.
Mwandishi na mtafiti wa masuala ya kihisia, Brené Brown, naye anaongeza mtazamo muhimu.
Katika kitabu chake: Atlas of the Heart, anaandika: “Hatuna ujuzi wa kutosha wa lugha ya hisia, na hilo linatuzuia kujielewa sisi wenyewe na kuelewana.” Anaeleza kuwa jamii mara nyingi huwalea wanaume na wanawake kwa misingi tofauti ya kihisia. Wanaume hufundishwa kuficha au kudhibiti hisia, hasa huzuni na hofu, wakati wanawake hutiwa moyo kuzionyesha.
Matokeo yake ni kuwa wanawake wengi huonekana “wenye hisia kupita kiasi,” ilhali wanaume huonekana “baridi” au “wasiojali.”
Ukweli, kwa mujibu wa waandishi hawa, ni kuwa wote wanahisi kwa kina, lakini njia za kueleza hisia hizo ndizo hutofautiana.
Kutambua tofauti hizi kunasaidia kupunguza lawama na kuongeza huruma katika uhusiano.
Maneno dhidi ya maana iliyojificha
Tofauti za kihisia zinaenda sambamba na tofauti za kimawasiliano. Deborah Tannen, mtaalamu wa isimu na mwandishi wa kitabu: You Just Don’t Understand, anaeleza kuwa wanaume na wanawake hutumia lugha kwa malengo tofauti.
Anasema wanawake hutumia mazungumzo kujenga ukaribu, kushirikiana hisia na kuthibitisha uhusiano.
Ndiyo maana mazungumzo marefu na ya kina yanaonekana kuwa muhimu zaidi kwao. Wanaume, kwa upande mwingine, mara nyingi hutumia lugha kama chombo cha kubadilishana taarifa au kuonyesha uwezo na hadhi.
Hii inasababisha hali ambapo mwanaume anaweza kutoa suluhisho la haraka, wakati mwanamke alihitaji kusikilizwa tu.
Gray analigusia pia suala hili anaposema: “Mwanamke anapozungumza, si lazima awe anaomba ushauri.”
Kauli hii imekuwa maarufu kwa sababu inaeleza chanzo cha migogoro mingi ya kila siku. Mwanaume anapojaribu kurekebisha tatizo mara moja, mwanamke anaweza kujisikia kutosikilizwa au kupuuzwa kihisia.
Kimtazamo hali hii inaonekana hata katika familia nyingi za Kiafrika na mijini. Wanandoa wanapokaa mezani, mmoja anataka kuzungumza kuhusu siku yake na hisia zake, mwingine anajibu kwa sentensi fupi au ushauri wa haraka.
Bila uelewa wa tofauti hizi, mawasiliano yanageuka kuwa chanzo cha majeraha badala ya daraja la ukaribu.
Kujifunza lugha ya jinsi nyingine
Mwandishi, Gary Chapman, kupitia kitabu chake: The Five Love Languages, anaweka msisitizo katika kujifunza namna mwenzako anavyopokea na kuwasiliana upendo.
Anaandika: “Watu huwa wanaeleza upendo kwa namna wanayotamani kupendwa.” Kauli hii inaeleza kwa nini wanaume na wanawake mara nyingi huhisi hawapendwi, ilhali wote wanajitahidi.
Chapman anaonyesha kuwa tofauti za kihisia na kimawasiliano si tatizo lenyewe; tatizo ni kutojifunza lugha ya mwenzako.
Mwanamke anaweza kuonyesha upendo kwa kuzungumza na kushiriki hisia, wakati mwanaume anaonyesha upendo kwa vitendo au kutatua matatizo. Bila uelewa, kila mmoja huhisi jitihada zake hazithaminiwi.
Brené Brown anasisitiza kuwa uelewano huu unahitaji ujasiri akisema: “Udhaifu wa kihisia ndio mahali uhusiano huzaliwa.”
Hii ina maana kuwa wanaume na wanawake wanahitaji ujasiri wa kusema wanachohisi na wanachohitaji, hata kama ni tofauti na matarajio ya kijamii. Mwanaume anapokubali kuzungumza kuhusu hisia zake, na mwanamke anapokubali kwamba si kila tatizo linahitaji mazungumzo marefu, pengo la mawasiliano linaanza kufungwa.
Kwa jumla, tofauti za kihisia na kimawasiliano kati ya wanawake na wanaume si ishara ya nani ni bora au dhaifu.
Ni matokeo ya malezi, tamaduni na hata biolojia. Katika jamii inayobadilika kwa kasi, ambako majukumu ya kijinsia yanachanganyika, uelewa huu unakuwa muhimu zaidi.
Kuelewa siyo kukubaliana kila wakati, bali ni kusikiliza kwa nia ya kuelewa. Hapo ndipo uhusiano unapopata nafasi ya kukua, badala ya kuvunjika kwa misingi ya kutoelewana.