London, England. Shughuli ni pevu. Ndicho unachoweza kusema kufuatia mchakamchaka wa mechi za Ligi Kuu England zitakazopigwa wikiendi hii.

Huko Emirates, leo kutakuwa na balaa zito, wakati Arsenal itakapokipiga na Chelsea, mechi itakayohusisha vita mbili, ile ya kusaka ubingwa na nyingine ya kufukuzia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Arsenal ipo kwenye mbio za ubingwa, hivyo itahitaji ushindi kwenye mechi hiyo ya dabi ya London ili kuendelea kutanua pengo la pointi kwenye kilele cha msimamo wa ligi, lakini Chelsea nayo ikihitaji ushindi ili kuhakikisha inaendelea kubaki ndani ya Top Four. Patamu hapo.

Arsenal imeweka pengo la pointi mbili dhidi ya Manchester City baada ya timu hiyo chini ya kocha Pep Guardiola kuichapa Leeds United bao 1-0 jana, Jumamosi.

Kwa upande za mechi nyingine za leo Jumapili, ukiweka kando kipute cha Arsenal na Chelsea, vita nyingine ya Top Four itawahusu Manchester United watakaokuwa uwanjani Old Trafford kukipiga na Crystal Palace, huku Fulham ikiwa na kasheshe la kukutana na wababe wenzao wa London, Tottenham Hotspur wakati Brighton itakuwa nyumbani kuonyeshana ubabe na Nottingham Forest.

Man United inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye mchezo wake kutokana na kiwango bora ambacho wamekuwa nacho kwenye michezo kadhaa iliyopita chini ya kocha mpya Michael Carrick.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *