GEITA: SERIKALI inakusudia kuunda chombo maalum kwa ajili ya kuimarisha ulinzi na kudhibiti shughuli haramu ikiwemo uvuvi haramu ndani ya ziwa Victoria, mito na vyanzo vingine vya maji.
Waziri wa mifugo na uvuvi Balozi Dk Bashiru Ally alisema taarifa hiyo juzi akiwa ziarani kukagua miundombinu ya uvuvi pamoja na soko la dagaa la Chato Beach Wilayani Chato Mkoani Geita.
Balozi Dk Bashiru amesema uamuzi huo unakuja kwa kutambua kuwa uvuvi haramu unarudisha nyuma mipango ya serikali katika kukuza sekta ya vuvuvi kuongeza maduhuli kupitia sekta hiyo.
Amesema wataalamu wa wizara hiyo waliopelekwa wilayani Chato kutoa elimu kwa vitendo wamebaini uwepo wa wimbi kubwa la uvuvi haramu hali inayoahitaji hatua za haraka kudhibiti.
“Chombo kile kitakuwa kinafanya kazi kwa nguvu zaidi, kwa sababu tutakuwa na raslimali watu, tutakuwa na raslimali fedha, na nyenzo na zana za kisasa.
“Tutatumia teknolojia ikiwemo ndege nyuki hakuna atakayepenya, tutasimama ndani ya ziwa na nje ya ziwa, mpaka kwenye maghala”, amesema Balozi Dk Bashiru.
Balozi Dkt Bashiru ametahadharisha wale wote ambao wameficha nyenzo haramu za uvuvi wakati wa oparesheni huku wakisisitiza kuwa serikali imeweka mitego ya kuwanasa wote.
Amesema mipango ya ulinzi na usalama wa ziwa Viktoria ni endelevu na hivo nyenzo zote za uvuvi haramu zinaendelea kudhibitiwa na kuteketezwa kwa kuwa ni adui wa mazalia ya Samaki.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya ulinzi wa rasilimali za uvuvi Wilaya ya Chato, Furaha Bulonga amethibitisha wimbi kubwa la uvuvi haramu lilibainika katika oparesheni ya Februari 25, 2026.
Amesema oparesheni hiyo iliyofanyika katika mwalo wa Matofali uliopo Kata ya Makulugusi Wilayani Chato ulinasa jumla ya nyavu haramu 60 zinazotumika kinyume cha sheria.
Amesema pia jumla ya matenki ya mafuta 33, Mitumbwi 60 na Injini 40 za kupachikwa kinyume na Sheria na taratibu za uvuvi zimekamatwa na wahusika kuchukuliwa hatua.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Chato kushirikiana kikamirifu na maofisa uvuvi kuhakikisha wanasimamia maelekezo ya serikali katika sekta ya uvuvi.
