Timu ya Alicia Keys, DMF watua AmanaTimu ya Alicia Keys, DMF watua Amana

DAR ES SALAAM: Timu ya wawakilishi kutoka Taasisi ya Keep A Child Alive, ya msanii Alicia Keys, imewasili Tanzania ikiwa na lengo la kushiriki uzinduzi wa jengo la kisasa la kuhudumia watoto njiti Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza.

Baada ya kuwasili nchini, timu hiyo ilielekea moja kwa moja katika Hospitali ya Amana Hospital ambako iliwatembelea wagonjwa, hususan watoto njiti, kuwajulia hali pamoja na kutoa zawadi mbalimbali.

Vilevile, walipata fursa ya kujionea mazingira ya utoaji wa huduma za afya kwa watoto njiti na kujadiliana na uongozi wa hospitali kuhusu mahitaji ya kuboresha huduma hizo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Kiongozi wa Wawakilishi wa taasisi hiyo, Antonio Ruiz-Gimenez, alisema uzoefu wake binafsi wa kupata mtoto njiti umekuwa chachu ya dhamira yake ya kusaidia watoto wanaozaliwa katika mazingira hayo, hususan katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

Alibainisha kuwa taasisi yao itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kuimarisha huduma za watoto njiti.

Kwa upande wao, wawakilishi wa Doris Mollel Foundation (DMF) walieleza kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya juhudi za muda mrefu za taasisi hiyo katika kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini.

Jengo la kisasa la kuhudumia watoto njiti lenye viwango vya Kimataifa lililojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba, mkoani Mwanza, limefadhiliwa na Doris Mollel Foundation chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji wake, Doris Mollel.

Jengo hilo linatarajiwa kuzinduliwa leo, Februari 28, 2026, na linatarajiwa kuongeza kwa kiasi kikubwa ubora wa huduma za afya kwa watoto njiti katika eneo hilo na mkoa kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *