Nyoro afichua athari za uchumi KenyaNyoro afichua athari za uchumi Kenya

MASUALA ya kiuchumi nchini Kenya si ya kuwakatisha tamaa Wakenya pekee, bali pia yanawashangaza wachambuzi wa uchumi kadiri siku zinavyosonga kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Kiharu, Kaunti ya Murang’a, Ndindi Nyoro. Baada ya kuchambua kwa kina matamshi ya Nyoro, imebainika kuwa changamoto za kiuchumi zinazoikabili Kenya kwa sasa, hususan suala la ulipaji wa deni la taifa ni kubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa awali.

Kwa mtazamo wa mchambuzi wa uchumi, hoja zake zinaibua maswali muhimu kuhusu mwelekeo wa sera za kifedha nchini.Nyoro anadai kuwa Kenya iko ukingoni mwa mporomoko wa kiuchumi unaochochewa na uuzaji wa mali za kimkakati za serikali, ukopaji uliopitiliza na mbinu za ufadhili zisizo wazi (off-book financing) zinazofichwa chini ya majina mapya kama Mfuko wa Miundombinu (Infrastructure Fund).

Amesema serikali inaweka mbele maslahi ya kisiasa ya muda mfupi hasa maandalizi ya uchaguzi wa 2027 badala ya kuzingatia uimara wa uchumi wa muda mrefu kwa manufaa ya wananchi. Nyoro anaonya kuwa kwa sasa Kenya inakopa takribani shilingi trilioni 1.25 kwa mwaka kwa hesabu halisi (net borrowing), sawa na takribani shilingi bilioni 3.5 kila siku.

Analinganisha hali hiyo na kipindi cha utawala wa Rais wa zamani Mwai Kibaki akisema kuwa kiwango hicho kilikopwa ndani ya takribani miaka kumi. Kwa mtazamo wake, kasi na ukubwa wa ukopaji wa sasa havijawahi kushuhudiwa na haviwezi kudumu kwa muda mrefu. Aidha amesisitiza kuwa takwimu hizo hazijumuishi madeni yanayolipwa upya (refinancing) hivyo kufanya kiwango halisi cha ukopaji kuwa kikubwa zaidi.

Mbunge huyo anahusisha mwenendo huo wa ukopaji na kile anachokiita uuzaji wa kimyakimya wa mali za umma. Anataja uuzaji unaoripotiwa wa hisa za National Social Security Fund (NSSF) katika East African Portland Cement kwa kampuni yenye uhusiano na Tanzania, akidai kuwa mali hiyo iliuzwa chini ya thamani yake halisi.

Anahoji kwa nini mwekezaji wa kigeni aone thamani katika kampuni ya ndani ambayo mfuko wa pensheni wa kitaifa haukuona sababu ya kuihifadhi. Kwa mtazamo wake, hali hiyo inaashiria kuingiliwa kwa maamuzi ya uwekezaji ya NSSF na kuhatarisha akiba za pensheni za wafanyakazi wa Kenya. SOMA: Siasa zayumbisha uchumi Kenya

Akifafanua zaidi,Nyoro anazungumzia kile anachokiita “neno jipya mjini” Mfuko wa Miundombinu akisema kuwa kimsingi ni chombo cha kuuza hisa za serikali katika kampuni za kimkakati zikiwemo Safaricom, pamoja na kuongeza mikopo mipya. Kwa mujibu wake, licha ya matumizi ya istilahi tata, kiini chake ni ama uuzaji wa mali za umma kwa bei ya chini au kuongeza mzigo wa deni.

Hoja nyingine anayoibua ni suala la “securitisation”yaani kukopa dhidi ya mapato ya baadaye. Nyoro anadai kuwa tayari Kenya imeweka rehani mapato ya ushuru wa mafuta wa miaka ijayo, hivyo kutumia mapema fedha zilizokusudiwa kufadhili ujenzi wa barabara kwa kipindi cha miaka saba ijayo. Pia anadai kuwa ushuru wa nyumba (housing levy) uko katika mchakato wa kuwekwa rehani kwa namna hiyo hiyo.

Kwa maoni yake, hatua hizi ni sawa na kukopa kwa jina tofauti na zinawaachia vizazi vijavyo mzigo wa kifedha. Akitolea mfano wa mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo wenye thamani ya shilingi bilioni 44.5, Nyoro anasema kuwa gharama halisi inaweza kufikia zaidi ya shilingi bilioni 140 baada ya kujumlisha riba kwa kipindi cha miaka 15.

Anatumia mfano huo kuonyesha jinsi maamuzi ya ukopaji yanavyoongeza mzigo wa kifedha kwa muda mrefu hasa yanapochochewa na misukumo ya kisiasa badala ya busara za kiuchumi. Zaidi ya hayo, anaonya kuwa Kenya iko katika hatari ya kufuata mkondo wa mataifa kama Zambia, Sri Lanka na Ghana, ambayo yamelazimika kupanga upya madeni yao au hata kushindwa kulipa (default) kutokana na viwango vya juu vya madeni.

Pia anahoji mantiki ya kutoza ushuru wa barabara (tolling) kwenye barabara kama ile ya Nairobi Nakuru ilhali serikali inaendelea kukopa na kuuza mali za umma. Kwa maoni yake, iwapo serikali inakusanya fedha kupitia mikopo na uuzaji wa mali, basi inapaswa kutoa miundombinu ya umma bila kuwaongezea wananchi mizigo mingine ya ushuru.

Kwa ujumla, hoja kuu za Nyoro zinajikita katika mambo matatu: ukopaji usiohimilika, kuweka rehani mapato ya baadaye na uuzaji wa mali za kimkakati za umma. Anaonya kuwa endapo nidhamu ya kifedha, uwazi na mipango ya muda mrefu havitarejeshwa, Kenya inaweza kujikuta katika mgogoro wa madeni unaofanana na ule uliowahi kuzikumba nchi nyingine zinazoendelea.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, mjadala huu unagusa kiini cha utawala bora wa rasilimali za umma. Mifuko ya pensheni ni hazina ya kizazi hadi kizazi na usimamizi wake unapaswa kuwa wa uwazi, uadilifu na kulindwa dhidi ya dosari zozote za kiuongozi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *