Tanzania yazidi kujiimarisha uzazi salamaTanzania yazidi kujiimarisha uzazi salama

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema serikali ipo tayari kuwezesha utekelezaji wa mpango wa kujenga wodi 27 za kulea watoto njiti nchini. Mpango huo utawezeshwa kupitia uratibu wa kitaalamu, upatikanaji wa maeneo ya ujenzi na ujumuishaji wa vituo hivyo katika mfumo rasmi wa afya ili kuhakikisha uendelevu wake.

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, amesema Rais Samia aliyasema hayo alipokutana na ujumbe wa taasisi ya Keep a Child Alive (KCA) ulioongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Antonio Ruiz-Giménez Jr., Ikulu jijini Dar es Salaam.

Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano katika kuboresha huduma za uzazi pamoja na afya ya mama na mtoto nchini, na kuweka msingi wa ujenzi wa wodi 27 za kisasa za kulelea watoto njiti Tanzania Bara na Zanzibar zitakazojengwa kwa viwango vya kimataifa. SOMA: Rais Samia kuzindua ripoti ya tafiti afya ya uzazi na mtoto

Ushirikiano kati ya serikali na KCA unalenga kuharakisha utekelezaji wa mpango huo kupitia ujenzi wa miundombinu bora, uwekezaji katika vifaa vya kisasa vya kulelea watoto njiti, mafunzo kwa wataalamu wa afya na usimamizi mzuri wa rasilimali za afya.

Rais Samia, ambaye pia ni kinara wa Umoja wa Afrika katika afya ya uzazi, mama na mtoto, alisema ushirikiano huo utaongeza upatikanaji wa huduma za uzazi salama, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika na kuimarisha mfumo wa afya ya mama na mtoto nchini.

Machumu amesema mpango huo utatekelezwa kwa ushirikiano na taasisi ya Doris Mollel Foundation, ukiwa na lengo la kuimarisha miundombinu ya afya ya uzazi, kuongeza upatikanaji wa vifaa tiba na kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga wanaozaliwa kabla ya wakati.

Rais Samia amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022. Katika kipindi hicho, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua kwa asilimia 36, kutoka 67 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000.

Amesema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji katika ujenzi wa vituo vya afya karibu na wananchi, kuongeza ajira kwa watumishi wa afya na kuimarisha upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba vya kisasa.Hata hivyo, amebainisha bado kuna changamoto katika kupunguza vifo vya watoto wachanga kutokana na upungufu wa wodi maalumu za watoto wachanga.

Ruiz-Giménez Jr amemshukuru  Rais Samia kwa ukaribisho na kueleza utayari wa KCA kuendelea kushirikiana na Tanzania kuimarisha huduma za afya, hususan afya ya mama na mtoto. KCA ilianzishwa mwaka 2003 na msanii na mwanaharakati wa kimataifa wa haki za binadamu, Alicia Keys.

Nchini Tanzania, KCA kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation imefanikisha ujenzi na uimarishaji wa wodi ya watoto wachanga katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza. Wakati huohuo, Rais Samia amewasili mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku moja.

Leo anatarajiwa kukutana na Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, ambaye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa mwaka wa Mahakama pamoja na Maadhimisho ya Miaka 20 ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao yake makuu jijini Arusha.

Mazungumzo yao yatalenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na ushirikiano kati ya Tanzania na Ghana, pamoja na kujadili masuala ya kikanda na kimataifa yenye maslahi ya pamoja kwa nchi hizo mbili na Afrika kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *