IDADI ya Watanzania wanaotembelea Makumbusho ya Jiopaki ya Ngorongoro-Lengai yaliyopo Wilaya ya Karatu mkoani Arusha imeendelea kuongezeka. Makumbusho hayo yalizinduliwa Oktoba 16 mwaka jana na Makamu wa Rais mstaafu, Dk Philip Mpango.

Jiopaki hiyo ni ya pekee katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya pili barani Afrika. Ofisa Uhifadhi Mkuu na Msimamizi wa Makumbusho ya Jiopaki ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Dk Agness Gidna, aliiambia HabariLEO kuwa mwitikio wa Watanzania wanaotembelea makumbusho hayo unaendelea kuwa mzuri.

Amesema katika mwezi Novemba mwaka jana, watu 575 walitembelea makumbusho hayo ambapo kati yao 568 walikuwa Watanzania. “Kwa mwezi Januari mwaka huu, watu waliotembelea makumbusho walikuwa 463 na kati ya hao Watanzania walikuwa 451,” alisema Dk Gidna.

Amesema makundi yanayoongoza kutembelea makumbusho hayo ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, vyuo pamoja na makundi ya jamii yakiwemo ya Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) na makundi ya kikabila yanayotembelea maeneo ya asili yao. Dk Gidna amesema moja ya mambo yanayowavutia zaidi Watanzania wanaotembelea makumbusho hayo ni maonesho mbalimbali, hususan teknolojia ya kisasa ya kusikiliza sauti za wanyama.

Ametaja vivutio vingine kuwa ni kuendesha baiskeli ndani ya makumbusho pamoja na ukumbi wa utamaduni uliopo katika eneo hilo. “Wanafunzi wa sekondari hufurahia zaidi taarifa za kisayansi kuhusu jiolojia ya eneo la Ngorongoro, hasa kuhusu volkano iliyotengeneza mabonde na milima tunayoiona leo, historia pamoja na chimbuko la binadamu,” alisema.

Kuhusu wageni wa nje wanaotembelea makumbusho hayo, alisema mwitikio bado ni wa kawaida ingawa idadi yao inaendelea kuongezeka. Amewataka Watanzania na wananchi wa Afrika Mashariki kutembelea makumbusho hayo kwa wingi kwa kuwa gharama kwa wakazi wa Afrika Mashariki ni nafuu. Amesema wananchi wenye umri wa miaka 16 na kuendelea hulipa Sh 5,900, watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 15 hulipa Sh 1,180 na watoto chini ya miaka mitano huingia bure.

Kwa wageni kutoka nje ya Afrika Mashariki wenye umri wa miaka 16 na kuendelea hulipa Dola za Marekani 35.40, wenye umri wa miaka 5 hadi 15 hulipa Dola za Marekani 11.80 na watoto chini ya miaka mitano huingia bure.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *