MKURUGENZI wa Sayansi wa Taasisi ya Afya Ifakara (IHI), Dk Ally Olotu, amesema taasisi hiyo imeendelea kushiriki katika tafiti na ubunifu mbalimbali unaolenga kufikia lengo la kutokomeza malaria nchini Tanzania kupitia uzalishaji wa ushahidi wa kisayansi na maendeleo ya teknolojia za afya.

Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, katika kituo cha IHI Bagamoyo, Dk Olotu amesema tafiti nyingi ambazo wanafanya zinalenga uelewa wa mwenendo wa vimelea vya malaria, maisha na tabia za mbu wanaosambaza ugonjwa huo pamoja na kubaini njia bora za kuudhibiti.

Amesema kupitia ushirikiano na Serikali, vyuo vikuu na wadau mbalimbali wa afya ndani na nje ya nchi, tafiti za IHI zimechangia maendeleo ya afua mbalimbali za malaria, ikiwemo matumizi ya dawa mseto ya Artemisinin-based Combination Therapy (ACT), kama vile Artemether-Lumefantrine (ALU) ambayo imekuwa sehemu muhimu ya matibabu ya malaria.

Dk Olotu amesema kwa sasa wanaendelea  kufanya tafiti za majaribio ya kitabibu na ufuatiliaji wa ufanisi wa dawa za malaria ili kuhakikisha tiba zinazotumika nchini zinaendelea kuwa salama na zenye ufanisi dhidi ya vimelea vya ugonjwa huo.

“ Tunaendelea kufanya tafiti nyingine za magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na yanayoibuka kwa lengo la kusaidia ugunduzi wa suluhisho za afya zitakazoboresha maisha ya wananchi”, alisema Dk Olotu. SOMA: Mkenda ataka Tanzania kuzalisha dawa , aagiza utafiti kupewa kipaumbele

Ameeleza kuwa taasisi yake imejenga uwezo katika maeneo mbalimbali ya utafiti, ikiwemo sayansi ya vimelea, ikolojia ya mbu, maabara za uchunguzi na majaribio ya kitabibu, hatua inayowezesha tafiti kufanyika kuanzia hatua za awali hadi kutathmini ufanisi wa afua za afya.

Kwa zaidi ya miaka 70 taasisi yake imekuwa ikitoa mchango katika tafiti za malaria nchini Tanzania na kimataifa, huku ikiendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutengeneza ushahidi wa kisayansi unaosaidia sera na mikakati ya kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *