
ALIYEKUWA Kocha wa Stand United ‘Chama la Wana’, Juma Masoud, amejiunga na Songea United ya Songea, mkoani Ruvuma, baada ya kuondoka kwa makubaliano ya pande mbili, Meja Mstaafu, Abdul Mingange, aliyeanza na kikosi hicho tangu msimu umeanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Masoud, aliyewahi kuifundisha FGA Talents kwa sasa Fountain Gate, amesemaamejiunga na timu hiyo hadi mwisho wa msimu huu, huku malengo yake makubwa ni kutengeneza kikosi cha ushindani, licha ya ugumu wa Ligi.
“Nafasi tuliyopo sio nzuri wala mbaya sana kwa sababu gepu la pointi na wenzetu ni ndogo, nimeingia katikati ya msimu huu, ingawa malengo yangu ni kuona timu inacheza vizuri, kutokana na aina ya wachezaji bora tulionao,” amesemaMasoud.
Msimu wa 2024-2025, Masoud akiifundisha Stand United, aliiongoza kumaliza nafasi ya tatu katika Ligi ya Championship na pointi 61, jambo lililoiwezesha kucheza mechi za ‘Play-Off’ za kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara, ingawa alikwama.
Stand United iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu msimu wa 2018-2019, ilianza kucheza ‘Play-Off’ ya kwanza kwa kishindo kwa kuiondosha Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya kikosi hicho cha mjini Geita kumaliza nafasi ya nne na pointi 56.