Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Abbas Tarimba amesema hajafurahishwa na usajili wa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo katika msimu huu.

Akizungumza baada ya mchezo wa jana dhidi ya Simba ambao umemalizika kwa suruhu, Tarimba amesema kuwa Yanga inahitaji kuwa na wachezaji wanaoendana na ukubwa wa klabu hiyo.

“Ukweli mimi sijafurahiwa sana na ‘scouting’ yetu. Yaani ‘scouting’ utafutaji wa wachezaji wazuri wanaofaa kucheza klabu kama Young Africans. Ambayo ni klabu ya 11 kwa ubora Afrika kwa viwango ambavyo vimetolewa leo au jana kitu kama hicho.

Beki wa kushoto wa Simba, Nickson Kibabage, akijaribu kumdhibiti kiungo mshambuliaji wa Yanga, Max Nzegeli, katika mechi ya Ligi Kuu ambayo imeisha kwa suruhu katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar. Picha na Yanga

“Sasa Unakuwa na wachezaji ambao ndio wanajitahidi ndio wanatafuta ushindi lakini wanapokutana na timu ngumu ni watu ambao wako ‘on and off’.

“Hiyo inatufanya viongozi wetu wajitahidi kufanya ‘scouting’ bora. Hivi tunavyopanda daraja kuwa timu ya 11 Afrika, elewa hata mashindano ya Afrika yatakuwa magumu,” amesema Tarimba.

Tarimba amesema kuwa kama Yanga itafanya usajili mzuri, anaamini itafanya vizuri katika misimu inayofuata kwenye mashindano ya klabu Afrika.

Amesema kuwa hana wasiwasi na uwezekano wa Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kwa vile wanao uwezo wa kufanya hivyo.

Kiungo mkabaji wa Yanga, Mudathir Yahya (kushoto), mwingine ni kiungo mkabaji wa Simba, Alasane Kante, wakiwa katika pambano la watani wa jadi, lililomalizika kwa suluhu visiwani Zanzibar. Picha na Simba

Tarimba amesema kuwa shauku yake kubwa ni Yanga kufanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa vile wao ni miongoni mwa klabu kubwa Afrika hivi sasa.

Katika mchezo wa jana uliochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Yanga na Simba zimetoka suruhu.

Matokeo hayo yameifanya Yanga iendelee kuongoza msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikifikisha pointi 29.

Simba imeendelea kuwa nafasi ya tatu ikifikisha pointi 24 huku nafasi ya pili wakiendelea kuwepo JKT Tanzania ambao wana pointi 28.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *