Dar es Salaam. Mshindi wa tuzo ya Oscar  Lupita Nyong’o amesema bado anapambana dhidi ya ugonjwa wa uvimbe wa kizazi, akibainisha umerudi tena kwa kasi baada ya kufanyiwa upasuaji.

Akizungumza na kipindi cha Today, staa huyo, 42, amesema mwaka 2014 alifanyiwa upasuaji na kuondolewa uvimbe wa sentimita 23, lakini sasa umegundulika anao zaidi ya 50cm.

“Safari hii nimeambiwa nina zaidi ya 50cm na narudi kukabiliwa na chaguo lilelile la  kufanyiwa upasuaji au kuishi na maumivu,” amesema Nyong’o.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, uvimbe wa kizazi ni uvimbe usio wa saratani unaoota ndani au kwenye kuta za misuli ya mfuko wa uzazi.

Hali hiyo inaweza kusababisha maumivu makali ya nyonga, kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi, hedhi ndefu isiyo ya kawaida pamoja na matatizo ya kibofu cha mkojo.

Nyota huyo aliyeigiza katika filamu ya A Quiet Place, Day One na The Wild Robot amesema bado hajafanya uamuzi wa hatua ya kuchukua kama kuendelea kuishi na maumivu au kufanyiwa upasuaji mwingine.

“Siko tayari kufanya uamuzi huo kwa sasa. Ni upasuaji mkubwa na una tishio kwa viungo vyetu vya uzazi naogopa sana,” amesema.

“Nadhani umefika wakati wa kuzungumza kwa sauti. Hili si jambo la kubezwa au kuonekana la kawaida kwa sababu tu ni la wengi.”

Hata hivyo, amesema kuamua kuzungumza hadharani kumempa nguvu mpya akiamini kuna wanawake wengi wanaopitia hali hiyo na wanashindwa kuzungumza na kusaidiwa.

“Nimepata jamii ya wanawake wanaopitia hali kama yangu. Kuna nguvu kubwa katika kuzungumza. Wanawake wengi wamesema na mimi pia nina changamoto hiyo, nikajua siko peke yangu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *