Dar es Salaam. Hakuna ubishi kuwa Master J ni kati ya watayarishaji muziki wenye mchango mkubwa katika kuikuza tasnia hiyo nchini akifanya kazi na wasanii mbalimbali katika studio yake ya MJ Records tangu miaka 1990.

Kwa takribani miaka 14 aliyokuwa studio kabla ya kustaafu, Master J ametengeneza nyimbo nyingi maarufu zilizoacha historia, na pia kuibua vipaji ambavyo baadaye viligeuka lulu katika soko la muziki. Fahamu zaidi.

1. Jina lake kamili ni Joachim Marunda Msafiri Kimaryo, hilo la ‘Master J’ alipewa na wasanii aliokuwa akifanya nao kazi miaka 1990 wakimaanisha Master wa Production, na ‘J’ ina inawakilisha Joachim.

MAST 01

2. Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu cha City University of London nchini Uingereza mwaka 1996, ndipo akaingia rasmi katika muziki lakini tayari alishaanza kujihusisha na mtayarishaji wake tangu 1994.

3. Chuo alisomea Electrical and Electronics Engineering ingawa anadai hakupenda hata kidogo, yeye alitaka kufanya muziki, hivyo alivyohitimu akawapatia wazazi degree yao, yeye akaenda kuanzisha studio ya MJ Records.

MAST 02

Hata hivyo, awali studio hiyo ilijukalikana kama MJ Production, alipofungua rekodi lebo na kuwasaini wasanii wa kwanza kabisa ambao ni kundi la Wagosi Wakaya, ndipo ilipozaliwa MJ Records.

4. Hiyo mwaka 1994 alipoanza kujihusishwa na utayarishaji muziki alikuwa na umri wa miaka 21, na alipoanza rasmi 1996 hakufanya kazi nyingine yoyote zaidi ya muziki hadi alipostaafu 2008 ikiwa ni takribani miaka 14 ndani ya studio.

MAST 03

5. Sababu ya kustaafu muziki ni ili kufanya kile alichosomea akifungua kampuni ya ujenzi lakini pale MJ Records aliwaacha watayarishaji muziki wengine akiwemo Marco Chali kabla ya kuja kuifunga kabisa studio hiyo.

6. Mdundo wa wimbo aliyoutengeneza ambao ulimfanya Master J kukuna sana kichwa, ni ule wa Professor Jay, Bongo Dar es Salaam (2001) akimshirikisha Lady Jaydee, ambaye pia ndiye alimtoa kimuziki.

Hadi sasa inaitaja ‘Bongo Dar es Salaam’ kama wimbo wake bora wa muda wote aliowahi kuutengeneza, na huu ulijumuishwa katika albamu ya kwanza ya Professor Jay, Machozi Jasho na Damu (2001).

MAST 04

7. Baadhi ya nyimbo nyingine kutoka katika mikono yake ambazo anaamini alizitendea haki, ni Dhahabu (Dully Sykes), Amekoma (Mhe. Temba), Nilikataa (TID  & Q Chief), na T shirt na Jeans (University Kona).

Nyingine ni Niite Basi (Joslin), Sintobadilika (Mike T), Nimekubali (Mez B), Sifai (Q Jay), Nalivua Pendo (Mwasiti), Nimemfukuza (Norichiko), Nimekusamehe (Bui Bui), Rudi Nyumbani (Makamua) n.k.

8. Master J anamtaja Mr. II Sugu kama msanii ambaye alikuwa akipata urahisi zaidi kufanya naye kazi. Wawili hao walianza kurekodi pamoja katika albamu ya pili ya Sugu, Ndani ya Bongo (1996).

MAST 05

9. Wimbo wa kwanza kwa Master J kutengeneza ni wa kundi la Deplowmatz ‘Are You Down/ R U Down’, na wa mwisho ni wake, Joslin ‘Niite Basi’ ambao ulioandikwa miaka miwili kabla ya kurekodiwa.

Ikumbukwe kundi la Deplowmatz ambalo lilianzishwa mwaka 1992 likijita katika muziki wa rap, liliundwa na wasanii kama Saigon, Trip Dogg, Dola Soul na Storm.

10. Akiwa miongoni mwa majaji wa Bongo Star Search (BSS) na aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi, Master J anamtaja Walter Chilambo kama msanii wake bora wa muda wote kutokea katika shindano hilo.

Mwaka 2012, ndipo Walter Chilambo aliibuka mshindi wa BSS, shindalo la kusaka vipaji vya uimbaji ambalo lilianza 2006 chini ya Benchmark 360 ambayo ni kampuni ya Madam Rita Paulsen.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *