
Kile ambacho kimefanyika katika Ligi Kuu Bara kwa msimu uliopita 2024-2025, kinabaki kuwa deni hivi sasa 2025-2026 iwe kwa wachezaji, timu na hata makocha.
Hiyo inatokana na takwimu zilivyo hadi kufikia sasa kulinganisha na ilivyokuwa msimu uliopita ambao Yanga ilitetea taji lake ikibeba kwa mara ya nne mfululizo.
Wakati Yanga inabeba ubingwa huo, ilimaliza na pointi 82 baada ya kucheza mechi 30, ikishinda 27, sare moja na kupoteza mbili, huku ikifunga mabao 83 yakiwa mengi zaidi kuliko timu nyingine na kuruhusu kumi, ambayo ni machache zaidi.
Nafasi ya pili ilishikiliwa na Simba ambayo nayo ilipoteza mechi mbili pekee kama Yanga, lakini ilikuwa na sare tatu ikishinda 25 ikimaliza na pointi 78, tofauti ni nne dhidi ya mabingwa.
Katika mabao, Simba ilifunga 69 na kuruhusu 13, ikishika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi na kuruhusu machache baada ya Yanga.
Jana watani hao wa jadi walikuwa uwanjani wakipambana kuwania pointi tatu katika mwendelezo wa ligi hiyo. Kabla ya mechi hiyo iliyowakutanisha kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, tofauti ya pointi ilikuwa tano. Yanga imekaa kileleni na pointi 28, Simba ya tatu ikikusanya pointi 23, zote zikicheza mechi kumi.
Mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo zimeshika kasi. Wakati Yanga na Simba zikiwa na mechi kumi kila moja kabla ya kukutana kwao jana, Azam na Singida Black Stars nazo zimeshuka dimbani sawa na wakongwe hao zikiwa bado hazijamaliza duru la kwanza.
Lakini timu zingine zina mechi nyingi zaidi zikianza duru la pili ambazo ni JKT Tanzania iliyoshuka dimbani mara 17, Namungo, Dodoma Jiji, Mtibwa Sugar na waburuza mkia KMC hizi zote zina mechi 16 kila moja
Zingine zilizomaliza duru la kwanza kwa kucheza mechi 15 ni Mashujaa na Coastal Union huku Fountain Gate, Pamba Jiji, Mbeya City na Tanzania Prisons zikicheza mechi 14, bado moja kumaliza duru la kwanza. TRA United ina mechi 13, bado mbili nayo kumaliza duru hilo.
Kitendo cha Yanga, Simba, Azam na Singida Black Stars zilizokuwa zikishiriki michuano ya CAF msimu huu zote kuishia makundi, vita ya Ligi Kuu Bara itakuwa kali sana kwani timu zote zinahamishia nguvu huko sambamba na Kombe la FA ili kuwania ubingwa.
Sasa basi, hali ikiwa hivyo, kuna wachezaji walikuwa na namba nzuri msimu uliopita katika ligi hiyo ambazo zimebaki kuwa deni kwao msimu huu kuzifikia au kuzipita na kuandika rekodi mpya.
Katika orodha ya wafungaji msimu uliopita, Jean Charles Ahoua wa Simba alimaliza kinara akifunga 16, akifuatiwa na Clement Mzize wa Yanga (14), kisha Jonathan Sowah, Steven Mukwala, Prince Dube na Lionel Ateba wakifunga 13 kila mmoja. Pacome Zouzoua akafunga 12.
Msimu huu, Fabrice Ngoy wa Namungo ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao mawili akiwa na kikosi hicho cha Wauaji wa Kusini, sasa ndiye kinara akifunga nane.
Kwa upande wa Ahoua, amefunga bao moja pekee, na sasa hayupo katika Ligi Kuu Bara baada ya dirisha dogo kutimkia CR Belouizdad ya Algeria, hivyo ameondoka na deni la mabao 15.
Kwa upande wa Mzize, mambo yamekuwa magumu kwani majeraha aliyopata Septemba 2025, yamemtibulia kwa kiasi kikubwa akishindwa kuitumikia Yanga ipasavyo. Hadi sasa anauguza jeraha la goti akiwa hajafunga bao lolote na kuna uwezekano akarejea siku chache kabla ya msimu kumalizika au ndio ikawa asionekane kabisa. Itategemea na uponaji wake.
Sowah kwa sasa yupo Simba akitokea Singida Black Stars, anafahamu ana deni la mabao 10 ili kufikia rekodi ya msimu uliopita aliocheza mechi 14 pekee za duru la pili kwani hivi sasa amefunga matatu.
Mukwala naye ameondoka Simba na kutua Al-Nasr Benghazi ya Libya huku akiwa amesepa bila bao, wakati Ateba yeye aliondoka Simba msimu uliopita uliomalizika akitua Al-Shorta SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Iraq.
Dube bado yupo Yanga, ana mabao yake matano kabla ya mechi ya jana, hivyo deni lake ni mabao manane, wakati Pacome kabla ya jana alikuwa na mabao matatu, bado tisa kufikia rekodi ya msimu uliopita.
Gibril Sillah aliyekuwa Azam, alifunga mabao 11 msimu uliopita, aliondoka mara tu msimu ulipomalizika akatua ES Setif ya Algeria ambayo amedumu kwa miezi sita na Januari 2026 amesajiliwa Al Ahly Benghazi ya Libya.
Elvis Rupia wa Singida Black Stars, alikuwa na mabao kumi, msimu huu ametupia mawili, bado manane kuweka mzani sawa.
Kinara wa msimu uliopita alikuwa Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam aliyemaliza na asisti 13, msimu huu pia ameuanza vizuri kwani kabla ya mechi ya jana, alikuwa pia kinara akiwa nazo nne sawa na Ibrahim Imoro wa Singida Black Stars na Duke Abuya anayecheza Yanga. Katika kuifikia rekodi ya msimu uliopita, Fei Toto anadaiwa asisti tisa.
Maxi Nzengeli alishika nafasi ya pili akiwa ana asisti kumi sawa na Pacome ambao wote wanacheza Yanga, msimu huu pia wote wanazo mbili kabla ya mechi ya jana. Bado asisti nane kuifikia rekodi yao.
Ahoua aliyemaliza na asisti tisa, ameondoka akiwa hana kitu, huku pia Dube kabla ya jana hakuwa na asisti wakati msimu uliopita alimaliza na nane.
Ellie Mpanzu wa Simba ni kama ameanza kwa kasi, kabla ya jana alikuwa na asisti tatu, wakati msimu uliopita aliocheza nusu alimaliza na sita.
CLEAN SHEET
Hapa kuna mabadiliko makubwa kama ilivyo katika mabao. Ukiangalia chati ya magolikipa waliokuwa wamecheza mechi nyingi bila ya kuruhusu bao ‘clean sheet’ kinara alikuwa Moussa Camara wa Simba akimaliza na 19, akifuatiwa na Djigui Diarra wa Yanga (17).
Chini yao alikuwepo Patrick Munthali (12), Yona Amosi (11) na Mohamed Mustafa (10) ambaye ndiye kipa pekee hakuwepo msimu huu baada ya kuondoka Azam.
Kwa sasa Camara unaweza kusema ameumaliza mwendo, kwani msimu huu amecheza mechi moja tu dhidi ya Fountain Gate na kupata clean sheet, baada ya hapo akaumia na kuondolewa kwenye orodha ya usajili wa wachezaji wa Simba, hivyo anatoka rasmi katika ushindani.
Aliyekuwa mpinzani wake, Diarra bado anaendelea kukichafua pale Yanga na kabla ya jana alikuwa na clean sheet tano akiendelea kuifukuzia rekodi yake ya msimu uliopita.
Munthali wa Mashujaa msimu huu ana clean sheet moja, akipigwa bao na Yona Amosi anayeidakia Pamba Jiji akifikisha clean sheet tano sawa na Diarra.
Munthali amepata ushindani wa namba kutoka kwa Erick Johora ambaye ndiye kinara wa msimu huu akiwa na clean sheet sita.
Mbali na Diarra na Yona, Ally Salim wa Dodoma Jiji aliyetua kikosini hapo msimu huu akitokea Simba, naye ana clean sheet tano.