Zurich, Uswisi. Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, amesema wachezaji wanaoziba midomo yao wakati wa mabishano uwanjani wanapaswa kupewa kadi nyekundu endapo kauli zao zitahusishwa na ubaguzi au lugha ya kuudhi.
Infantino amependekeza kuwepo kwa kile alichokiita “dhana ya kuwapo kosa”, akisema kufunika mdomo kunapaswa kuonekana kama dalili tosha kuwa mchezaji anasema jambo lisilofaa.
Kauli hiyo inakuja kufuatia sakata la ubaguzi lililomhusisha nyota wa Real Madrid, Vinicius Junior, na kiungo wa Benfica, Gianluca Prestianni.
Vinicius alimshutumu Prestianni kwa kumtukana kwa misingi ya kibaguzi katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwezi uliopita. Hata hivyo, uchunguzi bado unaendelea kubaini maneno halisi yaliyotamkwa, baada ya Prestianni kuonekana akifunika mdomo wake kwa jezi wakati wa tukio hilo.
Rais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Gianni Infantino, ambaye amependekeza iwapo mchezaji ataongea kwa kuziba mdomo atolewe nje ya mchezo kwa kuzaniwa amefanya kosa. Picha na Mtandao
Akizungumza na Sky News, Infantino amesema:
“Ikiwa mchezaji anafunika mdomo wake na kusema jambo lenye matokeo ya kibaguzi, basi anapaswa kufukuzwa uwanjani. Kufunika mdomo ni ishara ya kuficha jambo.”
Ameongeza kuwa haelewi sababu ya mchezaji kuficha mdomo kama hana jambo la kuficha. “Kama huna kitu cha kuficha, hufichi mdomo wako unapozungumza,” amesema.
Infantino amesisitiza kuwa soka linapaswa kuwa na msimamo mkali dhidi ya ubaguzi na kwamba hatua hizo zitasaidia kuwa na athari ya kuzuia matukio kama hayo siku zijazo.
Kiungo wa Benfica, Gianluca Prestianni, akizungumza kwa kuziba mdomo na nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr, kabla ya kuripotiwa kumtolea maneno ya kibaguzi mchezaji huyo raia wa Brazil, katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliopigwa Februari 17, 2026. Picha na Mtandao
IFAB kujadili mabadiliko ya sheria
Watunga sheria wa soka kupitia Bodi ya Kimataifa ya Vyama vya Soka (IFAB), wametangaza kuwa wataanza mashauriano kuhusu hatua za kukabiliana na ubaguzi, ikiwamo suala la wachezaji kufunika midomo.
Mabadiliko yoyote yatakayokubaliwa yanatarajiwa kuanza kutumika kabla ya Kombe la Dunia la 2026.
Katika mkutano wao wa mwaka, IFAB pia wameidhinisha mabadiliko kadhaa ya sheria ikiwamo hatua za kupunguza upotevu wa muda na maboresho ya matumizi ya VAR.
Kocha wa Benfica, Jose Mourinho, amesema endapo itathibitika kuwa mchezaji wake alitamka maneno ya kibaguzi, basi hatakuwa tena sehemu ya kikosi chake. Picha na Mtandao
Mourinho atoa msimamo
Katika sakata hilo, Kocha wa Benfica, Jose Mourinho, amesema endapo itathibitika kuwa mchezaji wake alikiuka misingi ya kupinga ubaguzi, basi hatakuwa na nafasi tena katika kikosi chake.
“Haki ya kudhaniwa kuwa hana hatia ni haki ya msingi ya binadamu,” amesema Mourinho, akisisitiza kuwa atasubiri matokeo ya uchunguzi kabla ya kuchukua hatua.
Vinicius, ambaye ni miongoni mwa wachezaji weusi mashuhuri duniani, amewahi kukumbana na matukio kadhaa ya ubaguzi katika maisha yake ya soka.
Sasa macho ya wadau wa soka duniani yanaelekezwa kwa FIFA na IFAB kuona kama mapendekezo ya Infantino yatapitishwa rasmi, hatua ambayo inaweza kubadili namna matukio ya mabishano uwanjani yatakavyoshughulikiwa siku zijazo.