Tabora. Mwenyekiti mpya wa Chama cha Wananchi (CUF), Mirambo Yusuf, ametangaza mkakati wa miezi sita kuanzia sasa wa kurejesha uhai wa chama hicho, ikiwemo kufanya maridhiano na kutatua migogoro ya ndani ili kurudisha imani ya wanachama.
Chama hicho kilifanya uchaguzi mkuu wa dharura kuanzia Februari 20, 2026, ili kupata uongozi mpya. Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi huo yameibua mgawanyiko miongoni mwa wanachama, ambapo baadhi wanatambua uongozi huo na wengine wanaupinga.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya kutengua uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, uliomweka madarakani Profesa Ibarahim Lipumba na wenzake watano.
Kwa mujibu wa Msajili, sababu ya kutengua uchaguzi huo ni kwamba Profesa Lipumba na wenzake hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya Katiba ya chama ya mwaka 1992; hivyo, mchakato ulipaswa kurudiwa.
Wananchi manispaa ya Tabora wakimsikiliza Mwenyekiti wa CUF Taifa, Mirambo Camil.
Uamuzi huo umeibua mgawanyiko ndani ya chama. Upande mmoja, ukiwemo wa Profesa Lipumba, ulipinga uamuzi wa msajili kwa madai haukuzingatia haki ya msingi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi kufanyika.
Upande mwingine, uliowasilisha malalamiko, uliunga mkono uamuzi huo ukidai uchaguzi wa Desemba 2024 haukufuata taratibu, hivyo ulipaswa kurudiwa ili haki itendeke.
Hata hivyo, baada ya kupatikana kwa uongozi mpya, chama kimegawanyika tena. Kundi moja halitambui uongozi huo, likidai haukupatikana kihalali kwa sababu baadhi ya wajumbe waliopiga kura hawakuwa halali.
Leo Jumatatu, Machi 2, 2026, Mirambo amepokelewa mkoani Tabora akitokea jijini Mwanza, ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu kuchaguliwa katika nafasi hiyo.
Ziara hiyo ina lengo la kujenga chama hicho na kuendelea kutatua migogoro midogo midogo ndani ya chama, ambapo akiwa hapo amezungumza na wanachama na wananchi katika ofisi za CUF zilizopo kata ya Gongoni, manispaa ya Tabora.
“Tutahakikisha kwanza maridhiano, migogoro yote ndani ya chama iweze kuisha, na njia pekee ya kufanikisha hilo ni kukaa kwenye meza ya maridhiano, tuzungumze tuone shida ilipo tuimalize,” amesema Mirambo.
Amesema mtandao wa chama unapaswa kurejeshwa tena, kwamba lazima uongozi uanzie chini, ngazi ya matawi, mpaka juu ili kuendelea kueneza sera na mikakati ya chama, ili watu wajue dhamira hasa ni kujenga nchi yetu na sio vinginevyo, na tena, mapato ya chama yanufaishe mpaka ngazi ya matawi.
Wananchi manispaa ya Tabora wakimsikiliza Mwenyekiti wa CUF Taifa, Mirambo Camil.
Amesema kuna baadhi ya wanachama wamejipa madaraka makubwa, kuna wengine wana nafasi ya mwenyekiti mkoa, lakini hao hao ni wenyeviti tena wilaya na hata kata, jambo hilo haliwezekani kwa sababu wanachama wengine wapo kwanini mtu mmoja awe na nafasi zaidi ya moja ndani ya chama.
“Sasa tunatarajia kuwa na misingi mizuri na shirikishi ya chama, kila mmoja ajisikie ana wajibu mkubwa wa kukitumikia chama chake kwa amani na kupewa nafasi ya kuonyesha uwezo alionao,” amesema.
Rehema Kabata, mkazi wa Tabora na mwanachama wa CUF, amesema hana mashaka na uongozi wa mwenyekiti huyo mpya ngazi ya Taifa, Mirambo, kwani ni mzoefu ndani ya chama na changamoto zilizopo anazijua na anajua namna ya kuzitatua.
“Kazi yetu sisi ni kumuunga mkono kiongozi wetu ili kuhakikisha tunarudisha ule uhai wa chama, kwa sababu kiukweli tumekua kimya, lakini pia hata uchaguzi uliopita hatukufanya vizuri, kwaiyo tunahitaji kujipanga,” amesema.
Ali Mheluka, mkazi wa Tabora, amesema pamoja na vipaumbele alivyo navyo kiongozi huyo, jambo kubwa ni kuangalia namna ya kuboresha maisha ya vijana, kutengeneza fursa za kiuchumi, na hiyo itasaidia taifa kusonga mbele haraka kiuchumi, ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma nyingine za kijamii.
“Tuwezeshwe vijana, maisha yetu yakue kwa haraka, lakini sera zao ikiwemo za mahitaji muhimu ya kijamii zitekelezeke, kwani wananchi huwa tunataka matendo na sio maneno tena,” amesema Ali.