MOROGORO: SHIRIKISHO wa Walimu Wanawake Wilaya ya Morogoro limewafariji wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika kitengo cha watoto wenye mahitaji maalumu katika Shule ya Msingi Njianne Kata ya Ngerengere, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Wanafunzi hao wamepatiwa msaada wa vyakula na mahitaji mengine muhimu ya shule ikiwemo mikeka ya namba na herufi ili kuwazesha kusoma kwa bidi
Mhasibu walimu wanawake, Jackine Mbise, amesema hayo kupitia risala iliyosomwa kwa niaba ya walimu wanawake wa wilaya hiyo mbele ya mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Kibena Kingo wakati wa ufunguzi kongamano hilo lililofanyika kata ya Ngerengere juzi.

Mbise amesema katika Shule ya Msingi Njianne ina kitengo cha watoto wenye mahitaji maalaumu wapatao 22 wanatoka katika familia zenye hali duni.
Amesema kuwa kati yao, watoto 12 ni wenye ulemavu wa akili, wanne ni wenye ulemavu wa viungo na mmoja ni mwenye ualbino.
Mbise amesema Watoto wanaoweza kujifunza ni 19 na watatu hawawezi kabisa kufika kituoni kutokana na changamoto kadhaa na hivyo ina mlazimu mwalimu anayesimamia kitengo hicho kujitokea kwa gharama zake kwenda kuwatembelea nyumbani kwa ajili ya kuwafanyia mazoezi ya viungo mara moja kwa wiki.

“ Sisi wanawake wa wilaya ya Morogoro tunampongeza Mwalimu Susan Gweba kwa kujitokea kwako kwa huduma hii muhimu kwa Watoto hawa “ amesema Mbise.
Mbise amesema kwa kutambua changamoto za watoto hao walimu wanawake wa wilaya ya Morogoro walifikia uamuzi wa kutoa mchango wa vyakula ambayo ni mchele , unga , sukari , mafuta ya kupikia , juisi, biskuti na mikeka ya namba na herufi kwa ajili ya kujifunzia.
Katika hatua nyingine wanawake hao wakiungana na viongozi wao kushiriki kupanda miti ya matunda na kivuli eneo la Shule ya Msingi Njianne ikiwa ni kampeni ya kutunza mazingira ili baadaye iwapatie wanafunzi matunda kwa ajili ya lishe bora.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Celina Kombani Memorial Foundation ,Lucy Kombani ambayo iliandaa kongamano hilo amesema ,taasisi hiyo imekijika kusaidia wanafunzi kielimu wenye kukabiliwa na changamoto mbalimbali wakiwemo wanaopata mimba awakiwa na umri ndogo.
Lucy ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Morogoro, amesema, taasisi itaendelea kuwasaidia wanafunzi wanaopata mimba wakiwa na umri mdogo kwa kuwapa elimu na ujuzi kwa kushirikiana na Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi (VETA) ili wautumie ujuzi wanaoupata kujiajiri wenyewe na kuondokana na utegemezi .
Kongamano hilo la wiki ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yenye kubeba kauli mbiu “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana : Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050 “ lilishirikisha vikundi mbalimbali vya wanawake wajasiriamali.