Dodoma.Taasisi ya Mifupa na Ubongo ya Muhimbili (MOI) imesema iko tayari kwa ajili kutoa huduma kwa wanamichezo watakaopatwa na madhira kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa fainali hizo ikiungana na Kenya na Uganda ambapo maandalizi yake yanaendelea.

Mkurugenzi wa MOI, Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya amesema Taasisi hiyo ina madaktari bingwa sita ambao wanatambulika na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Dk.  Mpoki amesema utaalamu wa madaktari waliopo na wasaidizi unatosha kutoa huduma kwa wachezaji kama itatokea changamoto yoyote kwa mtu kupata mvunjiko au shida nyingine itakayohitaji tiba bobezi.

“Tumejipanga vizuri kwa AFCON, wadaktari wetu wanatambulika na Shirikisho la Mpira na mmojawapo alisafiri na timu yetu kwenda Morocco kwenye AFCON kwa hiyo tutakuwa Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar tukiwa tayari kutoa huduma. Hatuwezi kutia aibu kwa nchi yetu,” amesema Dk Mpoki.

Mbali na kuwa na madaktari, Mkurugenzi huyo amesifu uimara wa vifaa walivyonavyo akisema ni vya kisasa vinavyokubalika kwenye utoaji wa huduma kwa viwango vya kimataifa.

Fainali za AFCON zilianzishwa mwaka 1957 na awamu iliyopita kwa maana ya AFCON 2025, zilifanyika Morocco zikishirikisha timu za taifa 24 barani Afrika huku Senegal ikiibuka bingwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *