DAR ES SALAAM:RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kesho Machi 3, 2026 katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa matenki 15 ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari wa habari leo Machi 2, 2026 na Waziri wa Uchukuzi, Makame Mbarawa, amesema kuwa mradi huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kupanua na kuboresha bandari hiyo ili kuimarisha nafasi yake kama lango kuu la biashara nchini na katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa sambamba na ujenzi wa matenki hayo ya mafuta, Serikali inaendelea na ujenzi wa gati namba moja lenye urefu wa mita 500, litakalokuwa na uwezo wa kupokea meli mbili kwa wakati mmoja, kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba takribani tani 50,000.
Ameongeza kuwa maboresho hayo yanalenga kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena kubwa zaidi, kupunguza msongamano wa meli na kuiwezesha Bandari ya Dar es Salaam kuwa miongoni mwa bandari zenye ushindani mkubwa zaidi katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Kwa mujibu wa Prof. Mbarawa, katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia jumla ya tani milioni 19.99 za shehena ndani ya miezi sita.
Serikali inalenga kufikia tani milioni 40 za shehena ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi mchango wa bandari hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.
